Njaa, ukame, siasa chafu zasababisha ongezeko la wakimbizi duniani

Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za binaadam, Jaji Imani Abood akihutubia majaji wa chama cha majaji wa Afrika wanaoshughlikia wakimbizi na wahamiaji leo katika kikao kinachoendelea Jijini Arusha 

Na Seif Mangwangi, Arusha

VIONGOZI wa nchi  za Afrika wametakiwa kujitafakari na kuja na
suluhisho la kudumu kuhusu tatizo la wakimbizi na wahamiaji ambalo limekuwa
likiongezeka kila siku kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinahitaji tafakari
ya kina.


Akizungumza kwenye ufunguzi wa
Mkutano wa Kimataifa wa majaji wa chama cha majaji wanaoshughulikia masuala ya
wakimbizi na wahamiaji leo Jijini Arusha Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki
za binaadamu (ACHPR), Jaji Imani Abood amesema tatizo la wakimbizi limekuwa likiacha
watu wengi katika simanzi.


Amesema maofisa wanaoshughulikia
uhamiaji katika nchi mbalimbali Afrika na duniani wanapaswa kujua kuwa watu
wamekuwa wakikimbia nchi zao kutokana na sababu mbalimbali na sio hiyari yao.


Jaji Imani amesema mbali ya siasa
kuwa sababu mojawapo inayofanya watu wengi kukimbia nchi zao mara baada ya
wanasiasa kutofautiana na kuibuka migogoro inayosababisha vita katika nchi
nyingi za Afrika lakini sababu zingine ni mabadiliko ya hali ya hewa.


“Kuna tatizo la mabadiliko ya hali
ya hewa ambayo katika miaka ya karibuni limekuwa ni tatizo kubwa sana, watu
wanahama nchi zao kutokana na ugumu wa maisha, wanakimbilia nchi zingine
kutafuta chakula, sasa watu wa uhamiaji wanatakiwa kujua hili,”amesema.


Amesema watu wanaoshughulikia
uhamiaji wanapaswa kujua kuwa hawa watu hawakimbilii katika nchi zao kwa
kupenda, bali kuna mambo magumu nyuma yao ndio sababu wanakimbia kutafuta
usalama wa chakula na maisha yao.


Jaji Imani amesema kupitia mkutano
huo, majaji ambao kazi yao kubwa ni kutoa maamuzi ya haki katika mahakama zao, watajadili
mambo mengi na kuja na tamko ambalo wataliwasilisha kwa watawala katika nchi za
Afrika.


Kwa upande wake Rais wa Chama cha
Majaji wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Duniani ambaye pia ni Jaji wa
mahakama ya Upeo nchini Kenya, Jaji Isaack Lenaole amesema nchi za Afrika
zinapaswa kujua sababu ya watu kuhama kabla ya kuzuia wasiingie katika nchi
zao.

Zaidi ya Majaji 200 wanachama wa Chama cha Majaji wa Afrika wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji wakiwa katika picha ya pamoja 


Amesema kutokana na ukame ambao
umezikumba nchi za Somalia na Ethiopia, zaidi ya watu 3200 wamekimbilia katika
nchi ya Kenya, ikiwemo wasomali 1800 na Waethiopia 1500 ambapo shida kubwa ni
njaa katika maeneo yao.

“Leo hii ukizuia wakimbizi na
wahamiaji wasiingie nchini kwako ni kwamba unataka wafariki jambo ambalo sio
sawa kibinaadam, hivyo tunapaswa kujadili suala la mipaka yetu na haki za wakimbizi
na wahamiaji na kuja na suluhisho la kudumu,”amesema.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha
Majaji wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Afrika, Jaji Dunstan Mlambo,
amesema warsha hiyo inafanyika ikiwa ni kuzikumbusha nchi za Afrika kuwa
kuhifadhi wakimbizi na watu wanaohitaji hifadhi za kisiasa ni haki za binaadam na
zinapaswa kuheshimiwa.

Amesema malengo ya warsha ni
pamoja na kuwajengea uwezo majaji kuhusu masuala ya wakimbizi na wahamiaji
katika nchi zao na kuwakumbusha majukumu yao ya kutoa haki. Pia katika warsha
hiyo majaji watajadili sheria za uhamiaji na kubainisha kasoro zilizopo ili
ziweze kufanyiwa mabadiliko.

Mkurugenzi wa utawala wa kisheria linaloshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji wa kiasiasi katika shirika la Konrad Adenauer nchini Ujerumani, Dr. Stefanie Rothenberger akitoa salamu za ufunguzi katika warsha hiyo