Paroko Parokia ya Moyo Safi Padre Festus Mangwangi aliwagawia wazee pesa ikiwa ni utaratibu wa kanisa hilo mara baada ya kumaliza misa ya kuwaombea na kula nao chakula cha pamoja |
*Wazee wasema vijana wanawaita ‘Malboro’
*Wanataka kuwaua, ili warithi mali
Na Seif Mangwangi, Arusha
Ukosefu wa maadili umeelezwa kuendelea kukua kwa kasi miongoni mwa vijana mkoani Arusha ambapo hivi sasa vijana wameanza kuwaita wazee wao majina ya kejeli kama ‘Malboro’, mfuko wa nailoni uliopigwa marufuku kuuzwa nchini.
Wakizungumza katika misa maalum ya kuwalisha wazee na kuwakumbuka kwa mambo mema ambayo waliyafanya wakati wa ujana wao katika kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria Unga Ltd, wazee hao walisema vijana wa hivi sasa wamekuwa wakichanganyikiwa kutokana na kukosa baraka za wazee wao.
“Sisi wazee tunaitwa Malboro, ule mfuko ambao Hayati Dkt Magufuli aliuzika, vijana wetu wakitaka kuoa mwanamke anaanza kumuuliza mpenzi wake Malboro zipo? akimaanisha kama sisi wazee ambao ni wazazi wa mwanaume bado tupo hai na kama tupo basi huyo mwanamke atahakikisha anatusambaratisha,”amesema mzee Raymond Msemo.
Hata hivyo amesema kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikiwadanganya kuwalipa wazee mafao ya kila mwezi kwa kuwa hawawezi tena kuendelea kufanyakazi na hivyo kuikumbusha kutimiza ahadi hiyo ili waweze kuishi maisha ya amani na kuepuka manyanyaso kutoka kwa vijana wao kwa kuwa watakuwa na kipato cha uhakika.
Amesema kukosekana kwa mafao kumekuwa kukisababisha kuishi maisha duni na kupelekea kudharauliwa na vijana waliowazaa wenyewe kwa kuwa wamekuwa tegemezi.
” Tunawasihi vijana wabadilike, watuheshimu wazee, vijana siku hizi wanakula dawa za kulevya, waache warejee kanisani, sisi zamani hatukuwa hivyo na ndio sababu tumebarikiwa ku niwa na umri mrefu zaidi,” alisema mzee Msemo.
Kwa upande wake Paroko wa Kanisa hilo Padre Festus Mangwangi, amesema mmomonyoko wa maadili miongoni mwao vijana umekithiri sana katika miaka ya hivi karibuni na hivyo kuwaomba wazee kutumia busara zao kukemea vitendo hivyo.
Akizungumza wakati akiendesha Misa takatifu kanisani hapo Padre Mangwangi amesema vijana wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo viovu kama ulevi, ushoga, wizi, ubakaji na ulawiti jambo ambalo limekuwa likimkasirisha Mungu.
“Siku hizi majanga hayaishi kwa sababu kila siku vijana wanamkasirisha Mungu kwa kufanya vitendo viovu, nawaomba wazee wangu kushirikiana na kanisa tukemee hivi vitendo,” amesema.
Padre Mangwangi amesema Kanisa hilo limekuwa na utaratibu wa kuhudumia wazee ikiwemo kukaa nao na kupata chakula mara mbili kwa mwaka na kwamba kupitia kanda 15 na jumuiya 74, kanisa limekuwa likihudumia zaidi ya wazee 300.
wazee wakifurahia pesa waliyokuwa wakipewa |
Amesema lengo la hafla hiyo ni kuwakumbusha watoto thamani ya wazee, kuwajali na kuwathamini.
” Wako watoto wenye nafasi na kazi nzuri lakini hawawataki wazee wao, tunafanya hili zoezi ili watoto wajue uthamani wazee wao, lakini pia ili waweze kutubariki tuweze kutekeleza majukumu yetu vizuri na ktk njia ipasayo,” Amesema
…na kuongeza,”tunapenda pia kuwaenzi wazee sababu wana nafasi kubwa ya kukemea maovu kwenye jamii, hasa watoto wao na wakisema watoto wanaweza kuacha,” Amesema.
Kwa mujibu wa Padre Mangwangi,hafla hiyo ambayo imekuwa ikifanywa na kanisa hilo pekee kipindi hiki pia imepata Ufadhilii kutoka katika familia ya Fabiene Jaquemet raia wa Uswis ambaye yuko nchini kama volunteer ambapo mbali ya wazee kupata chakula pia walipewa Tsh10,000 kila mmoja
Fabiene Jaquemet raia wa Swis akigawia wazee Tzs 10000 mara baada ya kumaliza misa ya kuwaombea na chakula |