Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ujio wa Rais Samia kesho Arusha |
Na Seif Mangwangi,Arusha
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kesho 2 Septemba 2023, anatarajiwa kuzindua jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU Tower), lililopo pembezoni mwa Barabara ya Arusha-Moshi Jijini Arusha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo, Jijini hapa Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema Rais Dkt Samia anatarajiwa kuwasili Jijini Arusha Jioni ya leo Septemba1,2023.
Amewataka wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais ambapo katika hafla hiyo mawaziri wote wanaoshughulikia masuala ya Mawasiliano na Posta watashiriki kwenye uzinduzi huo.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais wetu, lakini pia kuonyesha uzalendo hasa ukizingatia jambo linaloenda kufanywa ni la kimataifa, “amesema.
Mongela amesema huduma za posta nchini zimekuwa za kisasa zaidi kutokana na maboresho ya Hali ya juu yaliyofanywa chini ya uongozi wa awamu wa sita chini ya Serikali ya Rais Dkt Samia Hassan.
Awali Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema mawaziri wamekutana kujadili namna Bora ya kuiendeleza sekta ya huduma za posta na kukifanya Moja ya sekta zinazochangia maendeleo katika nchi za Afrika.
” Napenda kupongeza uamuzi uliofanywa kuandaa mkutano huu wa mawaziri ili kubadilishana uzoefu na kutafakari juu ya jukumu ambalo Huduma za Posta katika nchi zetu zinaweza kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kwa kuchangia maendeleo endelevu,”Amesema na kuongeza
“Ingawa, huu sio mkutano wa kisheria, nina imani kwamba maoni yatakayotokana na majadiliano haya yatatupatia fursa ya kuimarisha zaidi misingi imara ambayo huduma zetu za posta zitaendelea kustawi na kustawi,”Amesema.