Rais magufuli: tuimarishe umoja na mshikamano kuijenga sadc kuleta maendeleo kwa wananchi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifunga
rasmi mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC katika Ukumbi
wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere leo Jumapili Agosti
18, 2019.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa
Afrika(SADC) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof.Paramagamba Kabudi wakisaini Moja ya Mikataba iliyosainiwa
wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika Jijini Dar es Salaam,Tanzania.

Wakuu wa Nchi na Seriakali za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
Mwa Afrika (SADC) wakisaini mikataba ya makubaliano katika Mkutano wa Wakuu
wa Nchi na Wafalme uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa
Afrika(SADC), Dkt.Stagomena Tax na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Botswana,
Jan Sadek, Wakisaini Mikataba ya Programu za Maendeleo ya Viwanda SADC,
Uwezeshaji wa Biashara na Michakato ya Uimarishaji Viwanda Nchi za SADC, kazi
hiyo ilifanyika wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Jumuiya hiyo
uliofanyika Jijini Dar es Salaam,Tanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ali Mohamed
Shein na Makamu wa Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan wakifurahia jambo katika Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya
ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika Jijini Dar es
Salaam,Tanzania.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi
(kulia) na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt.Mohamed Gharib Bilal wakifuatilia
Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC uliofanyioka Jijini Dar es Salaam,
Tanzania.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika(SADC)
ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli, akihutubia wakati wa kufunga Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC
uliofanyioka Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia
Aksoni akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es
Salaam, Kathe Kamba, kabla ya Sherehe za Kufunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC uliofanyioka Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dkt.Bashiru Ally akisalimiana na
Mawaziri Wakuu Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John
Malecela(kulia) na Mizengo Pinda (Kushoto), kabla ya Sherehe za Kufunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC uliofanyioka Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
****************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
18.8.2019
RAIS Dkt. John Magufuli amewataka Wakuu Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea kuimarisha Umoja na Mshikamano na kuwa na sauti moja katika kusimamia maslahi mapana ya Jumuiya hiyo katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya hiyo, leo Jumapili (Agosti 18, 2019), Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alisema Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitaji ili kuharakisha jitihada za kuleta maendeleo katika jumuiya hiyo.
Aliongeza kuwa Umoja ni kiungo muhimu cha maendeleo katika ushirikiano wa Jumuiya yoyote, hivyo ili kuleta kasi ya mabadiliko ndani ya Jumuiya hiyo ni wajibu wa Nchi wanachama kuhakikisha inatumia vyema rasilimali zake pamoja na kuweka mkazo wa maazimio na agenda za Mkutano wa 39 kwa kutafakari masuala muhimu ya maendeleo.
Rais Magufuli alisema chini ya Uongozi wake, jumuiya hiyo itaendelea kusimama imara na kuwa na nguvu ya pamoja katika kutetea maslahi ya Nchi wanachama ikiwemo vikwazo ilivyowekewa Nchi ya Zimbabwe na kusema Viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kauli moja wameungana katika kuitaka jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
“Tutahakikisha kuwa jumuiya yetu inaondoa changamoto mbalimbali zinazozuia ukuaji wa uchumi ukiwemo vitendo vya rushwa na ukiritimba vinavyokwamisha sekta ya sekta ya biashara baina ya nchi zetu” alisema Rais Magufuli.
Akifafanua zaidi, Rais Magufuli alisema katika mkutano huo wa 39, Wakuu wa Jumuiya hiyo kwa pamoja wameweza kuwa na mjadala wa pamoja uliowawezesha Viongozi hao kutoa maoni, ushauri na michango yao na pamoja kusaini itifaki mbalimbali zilizoridhia agenda na mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema kutokana na kasi ndogo ya ukuaji uchumi iliyopo kwa sasa ndani ya jumuiya hiyo, aliwataka Viongozi hao kuhakikisha wanaweka mkazo katika kukuza na kuimarisha sekta ya miundombinu pamoja na kuboresha sera za kifedha na kiuchumi ili kukuza kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa kwa kila Nchi mwanachama.
Rais Magufuli pia aliitaka Sekretarieti ya Jumuiya kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya fedha hizo kutumika katika kuandaa makongamano, warsha na semina mbalimbali na sasa zielekezwe katika utekelezaji wa miradi inayoweza kuleta manufaa kwa nchi wanachama ndani ya jumuiya hiyo.
“Katika Bajeti yetu ya mwaka 2019/2020 tumepanga kutumia Dola Milioni 74, mchango wa Dola Milioni 43 zinazotolewa nan chi wahisani tunaweza kujenga vituo 17, nitafurahi kuona siku moja Sekretarieti ya jumuiya yetu ikiwaalika wanachama katika uzinduzi wa vituo hivyo” alisema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwakaribisha wawekazaji waliopo ndani ya SADC kuja kuwekeza katika miradi ya sekta mbalimbali iliyopo nchini ikiwemo nishati, madini, utalii, mifugo, kilimo pamoja na utalii kwani Tanzania imeweka mazingira bora na wezeshi kwa kwa ajili ya wawekezaji na wafanyabiashara.
Akizungumzia kuhusu maombi ya Nchi ya Burundi kujiunga na Jumuiya hiyo, Rais Magufulli alisema Sekretarieti ya jumuiya hiyo imepanga kutuma timu ya uchunguzi katika nchi hiyo kwa ajili ya kujiridhisha na masuala muhimu ya kimsingi yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kukubaliwa kwake kujiunga na Jumuya hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dkt. Stegomena Tax alisema Mkutano huo wa 39 wa SADC umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Nchi wanachama ambapo wameweza kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na maendeleo ya Nchi hizo.
Dkt. Tax alisema kuwa katika mkutano huo pia, Viongozi wa Jumuiya hiyo waliweza kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wa ndani katika Jumuiya hiyo ikiwemo Nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya Jumuiya hiyo (TROIKA) aliyokwenda kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.