Na Mwandishi wetu, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amekabidhi zaidi ya Shilingi Mil 640 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwa ni sehemu ya mikopo ya asilimia 10 ya Fedha zinazotokana na Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha .
Mongela akikabidhi mkopo huo katika hafla iliyofanyika katika ofisi za Kata ya Muriet , Tarafa ya Elerai alitaka wanufaika wa mikopo hiyo kutumia mikopo kwa kuanzisha shughuli zitakazobadili maisha yao na kuwa bora zaidi
Mkuu huyo alitaka kurejesha mkopo huo kwa wakati ili kuwezesha watu wengine kukopa na kujikwamua kutoka katika hali duni ya maisha.
Mikopo hiyo imetolewa na Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa ya robo ya Tatu na ya Nne ikiwa imelenga vikundi 48 vya Tarafa ya Elerai ambavyo ni vikundi vya wanawake 34 vilivyopata mkopo ya Tshs Milioni 364.8, vikundi vya vijana 13 vimepatiwa Tshs Milioni 273.08 na kikundi kimoja cha watu wenye Ulemavu Tshs. Milioni 3.
Mkuu huyo wa mkoa amesema fedha za mikopo hiyo zimetolewa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuanzisha shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujasirimali na hatimaye waweze kuongeza kipato na kuondokana na umaskini.
Mongela pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake kuwa Mhe. Rais ametoa mikopo hiyo ikiwa nikuwezesha wananchi anaowaongoza kuondokana na hali duni ya maisha baada ya kupata mkopo na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali .
Amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuendelea kutoa mikopo hiyo ambapo pia tayari Halmashauri hiyo imeweza kutoa mikopo kwa vikundi Tarafa ya Suye yenye thamani yaTshs million 504.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. Onesmo Mandike amesema kwamba Halmashauri itaendelea kutoa Mikopo hiyo kwa wakati na kutaka wananchi kujitokeza kuomba mikopo hiyo .
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jiji la Arusha, Bi. Tajiel Mahega, akitoa ufafanuzi wa mikopo hiyo alisema Halmashauri ya Jiji itaendelea kutoa mikopo hiyo na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watu na wajasirimali wanaomba mkopo lengo ikiwa nikuwawezesha kuanzisha Biashara zitakazobadili maisha yao kuwa bora na kuupa umaskini kisogo.