Serikali haitafunga mipaka ya burundi na congo-rc maganga

Meneja wa hotel ya Lake Tanganyika Beach ya mjini Kigoma Mohamed kimosa (kushoto) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Emanuel Maganga (katikati Mwenye mawani) jinsi hoteli hiyo ilivyochukua hatua mbalimbali za tahadhari za kujikinga na maambukizi ya Virus vya Corona.
……………………………………….

SERIKALI mkoani Kigoma imesema kuwa haijafunga mpaka wake na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na badala yake imeimarisha udhibiti kwa watu wanaoingia nchini kutoka nchi hizo kuhakikisha wanafanyiwa vipimo vya kutosha kubaini hali za afya zao.mwandishi wetu  Editha Karlo anaripoti toka Kigoma

Mkuu wa mkoa Kigoma Brigedia mstaafu Emanuel Maganga akizungumza baada ya kutembelea masoko, nyumba za kulala wageni na mahoteli makubwa mjini Kigoma kuangalia utayari wa watoa huduma hao kujikinga na virus vya Corona alisema kuwa udhibiti mkali umewekwa kwa wageni wanaoingia nchini kutoka nje.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa pamoja na kuangalia joto la mwili kwa kutumia vipimo vilivyopo mipakani, kuchunguza hali ya mwonekano wake pia historia ya msafiri huyo itachunguzwa kuona nchi alizotembelea kabla ya kuingia nchini na kwamba ikibainika ametoka kwenye nchi ambazo zinamaambukizi makubwa atawekwa karantini kwa siku 14.

Akizungumza baada ya ziara hiyo Mkuu wa mkoa Kigoma, Emanuel Maganga alisema kuwa ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na makundi mbalimbali katika kufuata maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na maambukizi ya Virus vya Corona na kusema kuwa hata hivyo kwenye maeneo ya masoko bado kazi kubwa inatakiwa kufanywa ili kuweka vizuri taratibu za udhibiti wa magonjwa.

Awali Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, shaban Magorwa alisema kuwa wamepita kwenye hotel zote kubwa mjini Kigoma na kukutana na watumishi wa hotelini hizo na kuwapatia elimu ya kujikinga na Virus vya Corona.

Sambamba na hilo Magorwa alisema kuwa kama itatokea kuna wagonjwa ambao wanahisiwa kuwa na maambukizi na kupaswa kuwekwa karantini zipo hotelini 12 ambazo zimebainishwa kwa watu hao kuishi wakati wakiendelea na taratibu za kuchunguzwa afya zao.

“Taratibu zote za kushughulikia udhibiti wa maambukizi ya Virus vya Corona zimezingatiwa ikiwemo kutengwa kwa eneo ambalo mgonjwa atakayepatikana atahifadhiwa wakati taratibu nyingine zikiendelea, lakini pia udhibiti wa wageni kutoka nje nao umepewa kipaumbele,”Alisema Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kufuatia mapungufu yaliyojitokeza kwenye masoko Mkuu wa mkoa Kigoma ametoa agizo kwa Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwailwa Pangani kuhakikisha mapungufu yanafanyiwa kazi ikiwemo uwepo wa maji ya kutosha muda wote kwenye masoko hayo.

Mwisho.