Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskasi Muragili akimpatia mtoto tone la chanjo wakati wa Kampeni maalum ya kutoa chanjo ya Polio katika Manispaa ya Singida |
Na Abby Nkungu, Singida
Jumla ya watoto 3,973 wenye umri chini ya miaka mitano wamepatiwa chanjo ya magonjwa mbalimbali katika halmashauri ya Manispaa ya Singida katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo, Dk Peter Sasi alitaja chanjo zilizotolewa kuwa ni kifua kikuu, surua, rubela, pepopunda, kifaduro, donda koo, kupooza, homa ya mapafu/Vichomi, kuharisha na homa ya ini.
Alieleza kuwa idadi hiyo ya watoto waliochanjwa ni sawa na asilimia 116 ya lengo la kutoa chanjo kwa watoto 3,430 katika kipindi hicho na kwamba lengo ni kuwajengea watoto hao kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Alifafanua kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kumetokana,
kwa kiasi kikubwa, na juhudi za wataalamu wa afya na wadau wengine kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu kwa kila mtoto kupatiwa chanjo.
“Si unajua sasa hivi kuna utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) ambayo pamoja na mambo mengine, imeweka mkazo juu ya afya bora kwa watoto walio chini ya miaka minane ili waweze kukua katika ukamilifu na utimilifu wao“ alieleza Dk Sasi.
![]() |
|
|
Aidha, alisema kuwa chini ya programu hiyo wadau kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo; hali iliyoongeza mwamko na mwitikio wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma na kupatiwa chanjo mbalimbali.
Dk Sasi alisema kuwa, kufanikiwa kwa zoezi hilo kumewakinga watoto husika na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kumesaidia kuwalinda watoto wengine wasiambukizwe magonjwa.
“Wito wangu, chanjo ni salama kabisa na hazina madhara yoyote kwani zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Wananchi wanapaswa kutambua hakuna Serikali duniani inayoweza kutoa chanjo yenye madhara kwa wananchi wake” alisisitiza.
Ingawa takwimu zinaonesha kufanikiwa kwa zoezi hilo, baadhi ya wazazi na walezi wanasema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo na kuondoa baadhi ya dhana potofu zilizojikita kwao.
“Ni kweli huenda maeneo ya mijini mwitikio wa chanjo ni mzuri lakini vijijini ni vyema utoaji wa elimu na hamasa ukaongezwa zaidi ili kila mtoto mwenye umri huo akapate chanjo” alisema Neema Daniel mkazi wa Mwankoko nje kidogo ya mji wa Singida na kuungwa mkono na Ramadhani Dule wa Utemini ambaye anasema viongozi wa mitaa, dini na mila watumike kuhamasisha.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, chanjo ni dawa ya kibaiolojia ambayo inalenga kukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Mpango wa Taifa wa Chanjo ulianzishwa mwaka 1975 ukiwa na lengo la kukinga watoto, wasichana na jamii kwa ujumla dhidi ya magonjwa yanayozuilika na chanjo. Hadi sasa, Mpango huo una jumla ya chanjo 14 dhidi ya magonjwa mbalimbali.