TAASISI ya utafiti na uzalishaji wa Miche bora ya Kahawa Tanzania (TACRI)kanda ya kusini imejipanga kuongeza uzalishaji wa miche hiyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima wa zao hilo katika Halmashauri 14 za kanda hiyo.Mwandishi Amon Mtega anaripoti
Akizunguza jana meneja wa TACRI kanda ya kusini Godbless Shao kwenye maonyesho ya sikuku za wakulima (Nanenane) zinazofanyika katika viwanja vya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma alisema kuwa taasisi hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji wa miche 2,565,000.katika kipindi cha msimu wa mwaka 2020/21 .
Shao amesema kuwa taasisi hiyo yenye makao makuu Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na kwa kanda ya kusini ni Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma inayofanya utafiti wa Miche bora ya Kahawa pamoja na kuizalisha kwaajili ya wakulima wa zao hilo katika Halmashauri 14 za kanda ya kusini kwenye msimu wa mwaka 2019/20 ilizalisha miche 1,943,240 ambayo yote iligawiwa kwa wakulima na kuwafanya wakulima hao waweze kuinuka kiuchumi kufuatia zao hilo la kibiashara.
Amesema kuwa miche hiyo ambayo hugawiwa kwa wakulima hao imekuwa ni miche bora ambayo haishambuliwi na magonjwa ya chulebuni na kutu ya majani (CBD)ambayo yatafanya wakulima kuto kuingia hasara tena kwaajili ya magonjwa hayo.
Aidha amesema kuwa matarajio ya kuongeza uzalishaji wa miche hiyo utaenda sambamba na mpango wa serikali ya awamu ya tano ambayo tayari imeshafikia katika uchumi wa kati wa viwanda ambao utasaidia Vijana wengi kupata ajira mbalimbali ikiwemo ajira ya kilimo ya zao hilo ambalo humuinua mkulima kwa haraka zaidi.
Hata hivyo Shao amesema kuwa taasisi hiyo imetoa mafunzo kwa maafisa ugani zaidi ya 42 ikiwemo na mafunzo ya kawaida kwa wakulima zaidi ya 952 jinsi ya kuitambua miche hiyo bora pamoja na namna ya kuihudumia bila kuingia garama ambazo zimekuwa zikimletea hasara mkulima wa zao hilo bila sababu za msingi.
Amefafanua kuwa licha ya mafanikio hayo bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kupanua wigo wa mafanikio yaliyokwisha kupatikana ili yawafikie wakulima wengi zaidi,Uhitaji mkubwa wa miche hiyo kwa kipindi kifupi kutokana na watu wengi kuhamasika kutokana na ubora wa miche hiyo,Uhaba wa maji kwenye bustani ya miche hiyo pamoja na maji safi ya kwa ajili ya usindikaji wa kahawa bora ambayo changamoto hiyo ipo karibu katika Halmashauri zote 14 zinazolima zao hilo kanda ya kusini.
Amesema kuwa changamoto nyingine kuwa bei kubwa za pembejeo za kilimo cha kahawa ikiwa ni pamoja na VAT ambayo ingeweza kufikiriwa na kuondolewa kabisa ili kuikwamua tasnia hiyo na kumfanya mkulima aweze kuendelea kunufaika zaidi katika kujiinua kiuchumi.
Hata hivyo meneja huyo ametoa wito kwa Halmashauri za Wilaya ambazo Wilaya zake zinalima zao la kahawa kuendelea kuhamasisha kilimo cha zao hilo ili kufanikisha kuinua mapato endelevu ndani ya Halmashauri hizo yatakayotokana na ushuru.
Maonyesho ya nanenane yamezidi kupamba moto katika viwanja vya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma mbapo vikundi mbalimbali vya wakulima na wafugaji vinaonyesha umahili wao katika uzalishaji hasa katika mwelekeo wa uchumi wa kati wa viwanda ambao tayari Serikali ya awamu ya tano imeshafikia.
MWISHO.