Naibu Spika Dkt Tulia Ackson Akikabidhi bendera kwa wanaopanda mlima Kilimanjaro maadhimisho ya miaka60 ya uhuru |
Na Seif Mangwangi, Kilimanjaro
zaidi ya washiriki 150 wameanza kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika.
kwa mujibu wa Kamishna msaidizi wa hifadhi ya Taifa TANAPA, Paschal Shelutete, idadi hiyo ya wapanda Mlima ni ya mara ya kwanza katika historia ya watanzania kupanda Mlima Kilimanjaro.
Shelutete amesema hamasa iliyofanywa na shirika hilo pamoja na kampuni ya utalii ya Zara, imeweza kusaidia watanzania wengi kujitokeza kupanda Mlima Kilimanjaro.
Akitoa salamu za Tanapa wakati wa kuzindua zoezi la kuanza kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro na kukabidhi bendera, Naibu Kamishna Tanapa, William mkelema amesema Tanapa imekuwa ikihifadhi na kulinda mlima Kilimanjaro tangu tulipopata uhuru mwaka 1961 ambapo tulikuwa na hifadhi tatu za Serengeti,Manyara na Arusha.
“Leo hii Tanapa tunajivunia mafanikio makubwa katika uhifadhi, leo hii ziko hifadhi 20 ikiwa ni, asilimia 11 ya eneo lote la nchi ya Tanzania tunaendelea kulitunza.l,” Amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Maliasili na utalii, Dkt Allan Kijazi amesema Wizara ka kushirikiana na Tanapa imeendelea kuhamasisha utalii wa ndani ijapokuwa mwitikio umekuwa mdogo tofauti na wageni kutoka nje ya nchi wanaotembelea hifadhi za Taifa.
“Wizara tumekuwa tukipokea maoni mengi ya kuboresha hifadhi ya mlima Kilimanjaro, hivi sasa tuna njia zaidi ya moja, hayo ni mafanikio makubwa katika miaka yote ya uhifadhi, utaona Kilimanjaro inashika namba mbili kuingiza mapato katika hifadhi zote 20,” Amesema.
Amesema shirika linaendelea kuboresha miundombinu ya hifadhi, ili kuhakikisha ekolojia yake inaendelea kuwepo na kusema kuwa mito mingi inayounda mto pangani maTuji yake yanatokea Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ambapo kupitia mito hiyo umeme umekuwa ulifikiwa.
Hata hivyo amesema Hifadhi hiyo imekuwa ikikabiliana na changamoto ya ulishaji wa mifugo msituni, kilimo pembezoni mwa hifadhi na ujangili lakini hata hivyo ushirikiano wa pamoja unatakiwa ili kukabiliana na changamoto hizo.
Akikabidhi bendera itakayokwenda kusimikwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro Naibu Spika Dkt Tulia Ackson amewataka watanzania kuwa wazalendo kama walivyofanya waasisi wa Taifa la Tanzania na kuhakikisha tunapata uhuru.
Kundi la watu 150 wanaopanda mlima Kilimanjaro kinaongozwa na Kanali Faustine Msumari wa Jeshi la wananchi Tanzania ambapo Disemba9 mwaka huu wanatarajia kupeperusha bendera ya Taifa katika kilele cha Uhuru katika Mlima Kilimanjaro.