Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameliomba Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za maji na nishati EWURA CCC kulishinikiza Shirika la umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Shinyanga kutoa huduma Bora na stahiki kwa Wananchi.
Wameyasema hayo wakati wa kikao cha baraza hilo na viongozi wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Shinyanga kilicholenga kuwajengea uwezo na kuwaelimisha ili waweze kufahamu haki na wajibu wao kwa wananchi juu ya upatikanaji wa huduma bora za maji na nishati.
Viongozi hao wameweka wazi kuhusu huduma zinazotolewa na TANESCO kwamba haziwaridhishi Wananchi na kwamba licha ya kuwepo malalamiko mengi lakini hakuna Ushirikiano wa kutosha unaotolewa na shirika hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya baraza la mkoa la ushauri la watumiaji wa huduma za maji na nishati EWURA CCC Shinyanga Kudely Sokoine ameziomba taasisi zinazojihusisha na utoaji wa huduma za nishati na maji kutambua wajibu wao kwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuzishughulikia.
“Ni vizuri wakajua unapokuwa kwenye taasisi ya umma kama TANESCO, SHUWASA na zingine kutoa huduma kwa wananchi siyo jambo la hiari wananchi wanalipa kodi kwahiyo wanastahili kupewa huduma zenye ubora na zinazokidhi viwango wasitoe huduma kwa mtazamo kama vile wanatoa msaada hapana wanatakiwa washuke chini kusikiliza changamoto walizonazo lakini pia wafanye kazi kwa kujitathmini ni kwa kiasi gani huduma wanazozitoa zinakidhi matarajio na viwango kutoka kwa wananchi”
“Wajumbe wamesema changamoto walizonazo na zinazowakabili wananchi nyingine zimepata majibu lakini nyingine mamlaka zimezichukua kama SHUWASA wamechukua changamoto zao wataenda kuzishughulikia lakini tutafuatilia kujua wamezishughulikia kwa kiasi gani lakini zingine tutaandika rasmi kwenda kwa TANESCO ili waweze kupokea na kuweza kuzishughulikia na waweze kutupa mrejesho lakini zingine siyo kwamba utatuzi wake ni wa papo kwa papo zinahitaji ufuatiliaji wa karibu na sisi kazi yetu itakuwa ni kuwasaidia wananchi na kuwaelekeza wapi waende wapate haki zao na tutahakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi katika matumizi ya huduma za nishati na maji”
Semina hiyo ya utoaji elimu kuhusu upatikanaji wa huduma zenye ubora, salama na stahiki imewahusisha madiwani wa kata zote na wenyeviti wa mitaa katika Manispaa ya Shinyanga.