Tari selian yagundua mbegu za kutibu upungufu wa nguvu za kiume

 

Na Claud Gwandu, Arusha

 

MCHANGANYIKO wa aina mpya ya mbegu za maharagwe  umeelezwa kuwa tumaini jipya kwa watu wenye
changamoto za uzazi, wakiwamo wanaume na wanawake wajawazito

 

Mbegu hizo mpya zilizogunduliwa hivi karibuni na
Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian(TARI-Selian) kilichopo Arusha  zinaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa
kurutubisha na kuongeza uzazi kwa watu wenye changamoto hizo.

 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mpango wa Maharage katika
Kituo hicho, Nestory Shida, matokeo chanya ya mbegu za maharage hayo yameanza
kuonekana katika mikoa kadhaa ambako sasa ni lulu.

 

Anasema mchanganyiko wa mbegu hizo uliogunduliwa
na kituo hicho mwaka 2018 hicho, umeonyesha matokeo mazuri katika mikoa ya Dodoma,
Singida, Iringa na Mbeya.

 

Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga
nayo imechangamkia aina hiyo mpya ya mbegu za maharage 

 

Mtafiti huyo alisema katika mafunzo ya waandishi
yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH)
yaliyofanyika jijini hapa hivi karibuni kwamba maharage hayo yana madini aina
ya chuma na zinki ambayo yanachochea hamu ya tendo la ndoa na kuongeza mzunguko
wa damu kwa wanawanake wajawazito

 

“Maharage hayo yanayoitwa Selian 14, 15 na Jesca yamekuwa
kimbilio la wengi katika mikoa niliyotaja kutokana na matokeo yake mazuri
katika masuala ya uzazi ambayo yamekuwa na changamoto nyingi na sasa ni
kimbilio la wengi,” Shida aliwaambia waandishi waliokuwa katika mafunzo hayo
walipotembelea kituo hicho na kuongeza:

 

“Mchanganyiko wa mbegu hizi umethibitisha kusaidia
kutibu tatizo la wanaume kushindwa kushiriki kikamilifu tendo la ndoa au
upungufu wa nguvu za kiume (ED) na kuboresha uwezo wa wanawake wajawazito
katika kutunza na kulea mimba.”

 

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, majaribio ya mbegu
hizo yamethibitisha kuwa madini yaliyo ndani ya mbegu hizo yana uwezo wa
kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume wenye upungufu lakini pia kusaidia mzunguko
wa damu kwa wanawake wajawazito.

 

Upungufu wa nguvu za kiume (ED) ni tatizo
linalowakabili wanaume wengi kutokana na sababu mbalimbali na linachangia
kuvunjika kwa ndoa nyingi.

 

Madini ya zinki yanasaidia kuongezeka kwa homoni
zinazosaidia kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la upungufu wa nguvu wakati
madini ya chuma yanasaidia mzunguko mzuri wa hewa ya oksijeni mwilini.

 

Aidha, Mtafiti huyo anaongeza kuwa aina hiyo ya
mbegu za maharagwe ni muhimu pia katika kusaidia tatizo la utapiamlo miongoni
mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano na kwa wanawake
wanaonyonyesha.