Tfra yatoa mafunzo na vyeti kwa wafanyabiashara wa mbolea

Meneja wa Mamlaka ya  Udhibiti Ubora wa mbolea Kanda ya Kaskazini Gothard Liampawe akitoa mafunzo kwa washiriki

Na Egidia Vedasto,

Arusha.

Wafanyabiashara na wasambazaji wa mbolea za viwandani wa mkoa wa Arusha wamepatiwa mafunzo ya namna bora ya utunzaji wa bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na namna bora ya kulinda afya zao katika utoaji huduma.

Akitoa mafunzo leo jijini Arusha Meneja Mamlaka Udhibiti wa mbolea Kanda ya Kaskazini Gothard Liampawe amesema mafunzo haya waliyopatiwa yatawasaidia kufanya kazi kwa ubora na si kwa mazoea.

Aidha ameeleza kwamba   wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka yanayouza mbolea na kugundua hawana elimu ya kutosha juu ya biashara ya mbolea ikiwa ni namna ya kuhifadhi mbolea kwa usahihi na kutoa elimu kwa wateja wao ambao ni wakulima.

“Mafunzo haya yataleta mabadiliko makubwa tofauti na hapo mwanzo, nategemea kuona tunakuwa marafiki na siyo maadui, na iwapo elimu haitazingatiwa basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yenu kwani itakuwa ni kukaidi na kututafuta ubaya”. Amesema Liampawe.

Washiriki katika mafunzo yaliyotolewa na TFRA leo Jijini Arusha

Liampawe ameendelea kufafanua kwamba wafanyabiashara wa mbolea wanatakiwa kukidhi matakwa ya sheria inayowahusu  namba 9 ya mwaka 2009 ili kuepuka usumbufu pindi wanapokaguliwa na mamlaka.

Ameongeza kuwa, wadau  wa mbolea ni pamoja na waingizaji mbolea, wafanyabiashara wa pembejeo, wazalishaji na hata wahasibu ilimradi wawe wanahusika na mbolea kwa ujumla wanatakiwa kupatiwa mafunzo kama ilivyofanyika leo na kupatiwa vyeti.

Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi Kanda ya Kaskazini Shelya Yusuph amesema mafunzo haya ni muhimu kwa biashara zao iwapo watayazingatia kwani yatasaidia kutimiza malengo na kuongeza wigo mpana wa biashara.

Washiriki na vyeti vyao katika picha ya pamoja na Wawezeshaji kutoka TFRA

Ameongeza kuwa katika ukaguzi waligunduua wafanyabiashara walikuwa wakifungua mifuko ya mbolea na kuiacha wazi, kitendo ambacho kinaharibu kiwango cha ubora wa mbolea.

“Pia niwakumbushe kuvaa koti na soksi za mikono wakati wa utoaji huduma, hii inawasaidia kujikinga na kemikali zinazotokana na mbolea, kuweka kumbukumbu za biashara na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wateja wenu” ameongeza Sheyla.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Agness Haule kutoka Can Feed  Us amesema mafunzo 

haya yamekuja kwa muda muafaka kwani hakuwa na elimu juu ya kuhifadhi mbolea kwenye  ghala na namna bora ya kutunza mbolea.

Mafunzo haya yamejumuisha washiriki 53 kutoka jijini Arusha na  kutunukiwa vyeti baada ya mafunzo waliyopatiwa kwa siku moja ambapo yataendelea kutolewa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Manyara.