Na Seif Mangwangi, Arusha
Watanzania wametakiwa kubadili mtindo wa maisha kwa kufanya mazoezi na kula mlo kamili ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza kama sukari na shinikizo la damu.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 14,2021 na profesa Andrew Swai ambaye ni mtaalam mbobezi wa magonjwa yasiyoambukiza hususani ugonjwa wa kisukari wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wanahabari wa Mkoa wa Arusha kuhusu magonjwa hayo.
Profesa Swai amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakisababishwa na mtindo wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, matumizi ya pombe, tumbaku na madawa ya kulevya, msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha.
Amesema watu wengi wamekuwa wakishinda darasani, ofisini, kuangalia runinha, kutumia lifti kupanda majengo marefu, kupanda magari na kutoshiriki michezo na ngoma za utamaduni.
Amesema ili kuepuka magonjwa hayo binaadam wa kawaida anatakiwa kila mlo anapokula uwe na makundi yote tano ya chakula, kula vyakula halisi, kutotumia mafuta mengi, kupunguza matumizi ya chumvi nyingi, kula kiasi ili kuepuka kunenepa.
” Jishughulishe kila siku kwa shughuli ambayo itakufanya utoke jasho kwa nusu saa, kutotamani vya wengine, kupata usingizi wa kutosha, epuka tumbaku na ulevi na chunguza afya yako angalau mara moja kwa mwaka,” amesema.
Amesema shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza (TANCDA), kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari wanaojihusisha na magonjwa yasiyoambukiza nchini, imekuwa ikitoa mafunzo kwa watu katika makundi mbalimbali ili kuwaepusha na magonjwa yasiyoambukiza ambayo katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakisababisha idadi kubwa ya vifo.