Moja ya gari lililokuwa limebeba mahindi likiwa limezuiwa |
*Yadaiwa wanataka risiti za ununuzi wa mazao
*Meneja asema hajapokea malalamiko rasmi
Na Seif Mangwangi, Manyara
WAFANYABIASHARA wanaosafirisha mazao kupitia Mkoa wa Manyara wamelalamikia mamlaka ya mapato TRA Mkoa wa Manyara kwa kile walichodai kuzuia magari yao na kuwasababishia hasara kubwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mkoani humo, wasafirishaji hao wa mazao kutoka katika mikoa ya Singida, Manyara, Shinyanga, Tabora na Mwanza wamesema TRA Mkoa wa Manyara wameanzisha utaratibu mpya wa kuwataka kuonyesha stakabadhi ya ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wadogo jambo ambalo halipo kisheria na halijawahi kufanyika nchini.
“Tangu juzi TRA mkoa wa Manyara wameanzisha utaratibu mpya wa kututaka kuonyesha stakabadhi ya ununuzi wa mazao kutoka kwa mkulima mdogo, tunajiuliza huyu mkulima yeye anatoa wapi mashine ya TRA hadi aweze kutoa risiti,”amehoji mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Salum Mabewa.
Amesema kuwa licha ya wao kuonyesha stakabadhi za ushuru waliolipa Halmashauri kama sheria inavyotaka pamoja na nyaraka mbalimbali za gari ikiwa ni pamoja na stakabadhi za malipo ya mizani bado magari yao yamezuiwa kuondoka mpaka wakabidhi risiti za ununuzi wa mazao.
Kutokana na sakata hilo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara hao, wafanyabiashara hao wamemuomba Waziri wa fedha kuingilia kati kunusuru hali hiyo kwa kuwa wameendelea kupata hasara kubwa kutokana na magari yao kuzuiwa na bidhaa kuchelewa sokoni.
” Tunamuomba Waziri wa fedha Dr Mwigulu Mchumba kuingilia kati suala hili kutokana na hasara kubwa tunayoendelea kuipata kwa magari yetu kuzuiwa hapa Manyara…sisi tunajaribu kufuata sheria za nchi lakini kila siku tunaletewa vikwazo, je, hivi ndio Mh Rais wetu aliagiza sisi wafanyabiashara tufanyiwe?,”alihoji Mabewa.
Hata hivyo Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Nicco Massawe amesema ofisi yake haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wasafirishaji hao wa mazao na kuwataka wafike ofisini.
Massawe amesema tatizo la ulipaji wa kodi ni kubwa sana kwa wafanyabiashara lakini pia kuna matapeli wengi wamekuwa wakitumia jina la TRA kunyanyasa wafanyabiashara hivyo amewataka waliokutwa na tatizo hilo kufika ofisini ili kueleza tatizo lako na kama kuna maafisa wa mamlaka hiyo waliokiuka utaratibu waweze kuwajibishwa.
” Naomba uwaeleze hao waliokutwa na tatizo hili wafike ofisi yoyote ya TRA walipo wataelewa malalamiko yao na sisi tutajulishwa, kama ni suala la elimu basi watapatiwa elimu lakini kama kuna afisa aliyekiuka taratibu atawajibishwa kisheria,”amesema.