Tra mkoa wa arusha wavuka lengo kwa kukusanya kodi sh 420.83 bilioni

 

Na Mwandishi Wetu
Arusha. 
Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) imezindua kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoa Arusha, huku ikijivunia mafanikio ya mkoa wa Arusha kwa kukusanya kodi  sh 429.83 bilioni mwaka 2019/20  na kuvuka lengo kwa asilimia 12.

Mkuu wa mkoa wa Arusha,Idd Kimanta alitoa taarifa hiyo jana, wakati akizundua kampeni ya elimu kwa mlipakodi na kuwataka wakazi wa mkoa wa Arusha, kujitokeza kupata elimu ya kulipa kodi kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Kimanta alisema licha ya mkoa wa Arusha kuvuka lengo la kukusanya kodi mwaka uliopita lakini, bado kuna fursa ya kukusanya kodi zaidi kama wafanyabiashara na wananchi wengi wakipata elimu ya kulipa kodi.

“pamoja na kukua kwa makusanyo bado kuna fursa zaidi ya kuimarisha ili kukusanya kodi zaidi baada ya elimu kutolewa mkoa mzima wa Arusha umuhimu wa kulipa kodi lakini pia taratibu za kulipa kodi”alisema

Kwa upande wake, Afisa kodi mkuu wa TRA,James Ntalika alitoa wito  kwa wafanyabiashara na wakazi wa Arusha, kujitokeza kupata elimu ya kulipa kodi na kuuliza maswali kwa maafisa ambao wamejipanga kutembea wilaya zote za mkoa wa Arusha.

Alisema katika kampeni hiyo hadi sasa wamebaini kuwa changamoto kubwa ambazo zinawakabili wafanyabiashara ni kutokutunza vyema kumbukumbu za biashara zao lakini pia kutokuweka  hadharani namba zao za mlipa kodi(TIN).

“tunawataka wafanyabiashara watunze vyema kumbukumbu, wasifunge biashara wanapotona sisi lengo letu ni kutoa elimu tu na tunawaomba kufika ofisi za TRA kupata msaada zaidi”alisema

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo inaongoza nchini kwa makusanyo makubwa ya kodi ya mapato kutoka katika sekta mbali mbali.

Mmoja wa walipa kodi mkoani hapa, Jeremiah Shirima alisema ongezeko la kodi Arusha linatokana na kuondolewa mfumo wa awali wa kudai kodi maafisa wa TRA kwa kuandamana na maafisa wa polisi.

“hivi sasa wanakuja kistaarabu wanakupigia mahesabu baada ya kuwapa kumbukumbu zako na unalipa kodi bila vitisho na kama kuna changamoto mnafikia makubaliana jinsi ya ulipahi tunaomba utaratibu huu uendelee”alisema Shirima.