Tusiruhusu mfumo mpya ununuzi wa korosho-majaliwa

WAZIRI MKUU amewaagiza Wakuu wa
Mikoa yote inayolima korosho nchini wahakikishe wanasimamia vizuri zao
hilo na wasiruhusu kuingizwa kwa mfumo mpya wa ununuzi ambao
haujaeleweka kwa wadau na wanunuzi.
“Mabadiliko  ya mifumo yalitolewa
na baadhi ya viongozi ambao sio waaminifu, Serikali iko macho
itawachukulia hatua viongozi wa vyama vya ushirika wasiokuwa waaminifu.
Tunataka mfumo wenye manufaa ndio utumike.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano,
Oktoba 2, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Mtwara baada
ya kukagua ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa
katika eneo la Mitengo, wilayani Mtwara.
Waziri Mkuu amesema msimu wa
korosho kwa mwaka huu unatarajiwa kutangazwa hivi karibuni, hivyo ni
lazima kwa wakuu wa mikoa inayolima korosho wakajiandaa vizuri ili
kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Waziri Mkuu ameendelea
kuwasisitiza wafanyabiashara kutojihusisha na ununuzi wa korosho kwa
njia ya kangomba.”Kangomba imepigwa marufuku, watakaojihusisha moto
utawawakia huko huko . Tunataka wakulima wenyewe ndio wanufaike”
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa
wakulima wa zao la korosho kuendelea kujiimarisha na wahakikishe
wanajiwekea akiba kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo kwa sababu.
“Serikali  itaendelea kusimamia zao hili ili wakulima wapate tija.”
Mapema, Waziri Mkuu ametembelea
ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini na kukagua kazi ujenzi
inayoendelea hospitalini hapo, ambapo amesema itakapomalizika
itawapunguzia wananchi safari ya kwenda Muhimbili kufuata huduma.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imejikita katika kuboresha
huduma mbalimbali za wananchi zikiwemo za afya, hivyo wananchi wa Kanda
ya Kusini watapata matibabu ya kibingwa karibu na maeneo yao.
“Hakuna mashaka wala wasiwasi wa
kupata huduma bora za afya kuanzia sasa na kuendelea kwa sababu Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imeendelea kuwezesha utaratibu mzuri wa kupata huduma za afya nchini.”
Ujenzi wa hospitali hiyo ya Rufaa
ya Kanda ya Kusini unatarajiwa kukamilika Agosti 2020 na kwa sasa
inajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa gharama ya zaidi ya
sh. bilioni 15 na tayari Serikali imeshatoa zaidi y ash. bilioni sita.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema
Serikali imetenga zaidi ya sh. Bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa
hospitali hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za
afya
Alisema historia ya mradi wa
ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa Mkoani
Mtwara ilianzia kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
cha Mkoa cha tarehe 16 Januari 1979. Halmashauri Kuu ilijadili na
kuazimia kuishawishi Serikali kujenga hospitali ya Rufaa ya Kanda ya
Kusini itakayohudumia Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Waziri Ummy aliongeza kuwa
hospitali hiyo inajengwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza  ilianza
mwaka wa fedha 2005/2006 kwa kazi ya upimaji wa mipaka na mwinuko wa
ardhi kupitia kampuni ya Beacon Consult Ltd kwa gharama ya sh.
26,000,000 na ilikamilika ndani ya siku 30 za mkataba. Kwa sasa ujenzi
huo upo katika awamu ya nne.
Awali,Waziri Mkuu alitembelea
kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo katika eneo la Msijute
mkoani Mtwara na kukagua kazi ya ubanguaji pamoja na kuzungumza na
watumishi wa kiwanda hicho ambao waliishukuru Serikali kwa kuhamasisha
ujenzi wa viwanda.