Unhcr laziomba tanzania na burundi kutowarudisha wakimbizi kwa lazima



Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR linaziomba serikali za Tanzania na Burundi kutowarudisha kwa lazima wakimbizi wa Burundi waliohifadhiwa Tanzania, linaripoti shirika la AP.

Waziri wa Mambo ya ndani Kangi Lugola

Katika taarifa yake, shirika hilo linaeleza licha ya kwamba usalama umeimarishwa Burundi tangu kuzuka ghasia kufuatia uchaguzi mkuu mnamo 2015 ” hali hairuhusu kushinikiza wakimbizi warudi Burundi”.

“Tunatoa wito kwa uwajibikaji wa serikali ya Tanzania na Burundi kutii majukumu ya kimataifa na kuhakikisha kwamba wakimbizi wowote wanaorudi, ni kwa hiari kwa mujibu wa makubaliano ya pande tatu yaliosainiwa Machi 2018.” AP limeinukuu taarifa hiyo ya UNHCR.

“UNHCR linaomba mataifa kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi anarudishwa Burundi kwa kushurutishwa na kwamba hatua zinachukuliwa kuifanya hali kuwa bora zaidi Burundi kuweza kuwapokea wakimbizi wanoarudi, ikiwemo kujenga imani na miradi kwa wanaoamua kurudi nyumbani.”

Serikali ya Tanzania imeeleza kwamba imefikia makubaliano na Burundi kuwarudisha wakimbizi makwao, na kusema kuwa hali ya kiusalama katika taifa hilo sasa imeimarika.

Kwa muda mrefu serikali ya Burundi imesisistiza kwamba taifa hilo li salama kwa raia wote wa Burundi kurudi nyumbani.
Kwa nini Tanzania inawakataa wakimbizi wa Burundi?

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola ametangaza kuwa wakimbizi 2,000 watarudishwa Burundi kufikia October mosi.

”Azimio la msingi lilikuwa kila wiki wakimbizi lazima wakimbizi elfu mbili wawe wanarejeshwa nchini Burundi lakini tulipokutana na Mamlaka ya Burundi tuligundua kuwa UNHCR ndio wamekuwa wakikwepa jukumu hilo likisema Burundi haina uwezo wakuwapokea wakimbizi 2000 kwa wiki” Waziri Lugola aliiambia BBC katika mahojiano ya kipekee.

Aliongeza kuwa serikali ya Burundi kupitia waziri wao wa mambo ya nje Pascal Barandagie waliwasilisha ombi lao kwa Tanzania kuelezea kutoridhishwa kwao na utekelezajiwa makubaliano waliofikia hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili na shirilka la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. Image caption Waziri wa Mambio ya ndani wa Tanzania, Kangi Lugola

Bw. Lugola anadai kuwa shirika hilo la wakimbizi lina ajenda ya siri kwasababu linaleta kisingizio ambacho sio cha kweli.

Mbali na maelezo iliyopata kutoka wizara ya Mambo ya nje ya Burundi kwamba nchi hiyo ni salama wazirri Lugola anasema kuwa imeridhisha kuwa wakimbizi hao watakuwa salama wakirudi makwao kwa sababu tangu mwaka 2015 hakuna hata mkimbizi mmoja aliyeingia nchini humo kutoka Burundi kwa kuhofia usalama.

Mvutano kati ya shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa mataifa na serikali ya Tanzania kuhusu suala la kuwaregesha makwao wakimbizi wa Burundi umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa sasa.

Mwezi Agosti mwaka mwaka 2017, Serikali ya Tanzania ililipatia shirika la UNHCR siku saba kuanza kuwarudisha wakimbizi wa Burundi ambao wanataka kurudi kwao kwa hiari, ama sivyo serikali ifanye zoezi hilo yenyewe.

Tanzania ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi kuliko nchi nyingine yoyote ile katika ukanda wa Afrika Mashariki.