Na Mwandishi Wetu, Arusha
Utata umegubika kufuatia kifo cha Mwanaapolo, Faraja Eliasi Metili (40) Mkazi wa Ilkiding’a wilayani Arumeru ambaye anadaiwa kuuawa na walinzi wa Mgodi wa Tanzanite one huku wenzake wanne wakishikiliwa na polisi wilayani Manyara baada ya kukutwa katika Mgodi huo uliosimamishwa uzalishaji na serikali.
Akiongea Kwa masikitiko ndugu wa marehemu, Karimu Elias ambaye ni kaka wa marehemu mara baada ya kufanyiwa uchunguzi mwili wa marehemu katika hospital ya Mount Meru, alisema kifo Cha Mdogo wake kimetokana na kipigo kutoka kwa walinzi wa Mgodi huo wakimtuhumu kuingia katika Mgodi huo kinyume na utaratibu.
“Mwili umefanyiwa uchunguzi hapa Mt.Meru tumeona unamajeraha makubwa na mbavu zimevunjika alipigiwa Sana inauma sana ndugu yetu kuuawa kinyama “alisema Eliasi
Eliasi analalamika kitendo Cha kuuawa Kwa ndugu yake akieleza kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria hata kama mdogo yake alikuwa na makosa hakihalalishi kuuawa ,ila angepelekwa kwenye vyombo vya sheria kama wenzake aliokuwa nao ambao wanashikiliwa na polisi Mkoani humo.
“Tunajipanga kwenda mahakamani kulalamikia kitendo Hicho na tunaomba Serikali iingilie kazi na wahusika wachukuliwe hatua”alisema.
Hata hivyo alienda mbali zaidi Kwa kudai kwamba iwapo serikali haita chukua hatua ,wao kama ndugu wa marehemu watachukua jukumu la kuvunja chungu ili wahusika wa tukio hilo waweze kuteketea mmoja baada ya mwingine na kwa Imani za kabila la kimasai kuvunjwa Kwa chungu ni hatua mbaya ambayo inaweza kuteketeza vizazi na vizazi vya familia za wahusika.
Naye kaka mwingine wa Marehemu John Silasi pamoja na mjomba wa marehemu,Samweli Ngalabale walisema wanasikitishwa na hatua ya jeshi la polisi Mkoani Manyara kukaa kimya wakati wahusika wanafahamika na wameiomba Serikali kuongilia Kati ili jambo Hilo lisijirudie.
“Sisi tunachojua kijana wetu ni mchacharikaji hatuwezi kujua kama aliingia katika Mgodi wa Tanzanite one “alisema Silasi.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi katika hospitali ya rufaa Mount Meru mkoani Arusha,na ndugu wa marehemu kukabidhiwa mwili huo ambao wamezika Leo kijijini kwao Ilkiding’a wilayani Arumeru huku marehemu akiacha watoto wawili na Mjane.
Kamanda wa polisi Mkoani Manyara, Harrison Mwakyoma alithibitisha tukio hilo na kueleza kwamba jeshi la polisi linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kuingia kinyume Cha sheria katika Mgodi wa Tanzanite one ambao Serikali imesimamisha uzalishaji na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
“Suala la Marehemu kuuawa na walinzi Mimi sifahamu ila polisi wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo”alisema Mwakyoma.
Wakati huo huo mfugaji anayejulikana Kwa jina Lobisingi Kairo(15)Mkazi wa Kijiji Cha Olorien wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha, ameuawa Kwa kuchomwa mkuki mgongo na kijana mwenzake mwenye umri wa Miaka 13 na kutolea upande wa Mbele.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jana majira ya saa mbili asubuhi baada ya kutokea mzozo wa kutoelewana wakati wakichunga mifugo.
Alisema baada ya tukio hilo marehemu alikimbizwa katika zahanati iliyopo katika kijiji hicho Kwa lengo la kuokoa Maisha yake lakini baada ya kufika katika zahanati hiyo waligundua marehemu ameshafariki dunia.
Masejo alisema jeshi la polisi Mkoani hapa linamsaka mtuhumiwa huyo ambaye jina lake linahifadhiwa baada ya kufanikiwa kikimbia baada ya tukio hilo.