Uturuki yamuonya jenerali haftar dhidi ya mashambulizi zaidi

Rais
wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan amesema nchi hiyo haitasita kumpa
fundisho Kamanda wa Wapiganaji wa Mashariki mwa Libya, Jenerali Khalifa
Haftar iwapo vikosi vyake vitaendelea kuishambulia serikali inayoungwa
mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli. 

Urusi
na Uturuki zilikuwa zinajaribu kupata mkataba wa kudumu wa kusitisha
mapigano ambapo mbabe huyo wa kivita wa Libya alitakiwa kutia saini
ambapo aliomba muda hadi leo Jumanne kufikiria suala hilo lakini baadaye
imefahamika kuwa ameondoka mjini Moscow bila kutia saini makubaliano
hayo.

Mazungumzo
ya jana Jumatatu yalitarajiwa kuweka rasmi mkataba wa muda wa kusitisha
mashambulizi ulioafikiwa siku ya Jumapili lakini mkataba huo
haukutekelezwa kikamilifu na kuna ripoti ya mapigano kuendelea nchini
Libya.

Taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lina serikali mbili pinzani.
Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na al-Serraj
mjini Tripoli na nyingine yenye makao yake katika mji wa Tobruk,
Mashariki mwa Libya inayoongozwa na Haftar.