Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wa pili kutoka kulia waliokaa akisikiliza hotuba ya ukaribisho iliyokuwa ikitolewa na DC wa Arusha Said Mtanda hayupo pichani |
Mkurugenzi Msaidizi Habari Maelezo Rodney Thadeus akitoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na wizara kwenye banda la wizara ya mawasiliano na Teknolojia ya Habari |
Afisa programu kutoka ubalozi wa Sweden nchini Stephen Chimalo akiteta jambo na mmoja wa washiriki katika mkutano huo |
Wageni mbalimbali wakisikiliza hotuba ya waziri Nape Nnauye |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Waziri wa Mawasiliano na teknolojia ya habari nchini Nape Nauye amekagua na Kuzindua maonesho katika mabanda ya wadau kuelekea kilele Cha Siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani Mei 3,2022 na kutoa rai kwa wanahabari kutumia fursa hiyo kujadili changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya habari ili zifanyiwe maboresho kupitia bunge.
Waziri Nape amesema ni jambo la kushukuru kwani bunge liko tayari kufanya mabadiliko kwa kutunga na kufuta Sheria zinazorudisha nyuma tasnia hiyo ambayo ni muhimili wa nne wa serikali hivyo ni muda muafaka kutumia majadiliano haya kupata muarobaini wa changamoto za sekta ya habari.
Katika hatua Nyingine Waziri Nape amezungumzia utajiri mkubwa uliopo katika nchi za bara la Afrika na ambao umekuwa chanzo kikubwa cha migogoro na vita katika nchi hizo.
Amewataka wanahabari kutumia kalamu zao kuelimisha umma kuhusu faida ya rasilimali hizo ili ziwe baraka kwa mataifa hayo badala ya kuwa chanzo cha migogoro.
“Kila mwanahabari anapaswa kufanya jukumu lake na kusimama imara kubadilisha changamoto zilizoko kwenye jamii kuwa fursa kwasababu ukitazama nchi nyingi zenye rasilimali ndiyo zinaongoza kwa migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, “Alisema Nape Nauye”.
Katika Hatua nyingine Waziri Nape amewataka wanahabari kutumia weledi wao kufuatilia na kuhabarisha umma juu ya mifumo mipya ya dijiti ukiwemo mfumo wa fedha wa Cryptocurrency ambao unashika Kasi duniani kwasasa.
Aidha amesema kuelekea kilele Cha siku ya vyombo vya habari duniani Vyombo vya habari vifanye kazi ya kulinda uhuru,rasilimali na tamaduni za mataifa yao.
Awali mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania, Deodatus Balile amesema tasnia ya habari imefurahishwa na namna serikali imeiheshimisha tasnia ya habari kwasababu Kuna hatua kubwa imepigwa hadi kuwa na Viongozi wa ngazi za juu za serikali ambao ni Wana habari hususani Mkurugenzi wa habari maelezo Gerson Msigwa na katibu mkuu wa wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari Jimmy Yonazi.
Kuhusu maboresho ya Sheria ya habari Balile ameomba serikali kuona namna ya kuanza kufanya maboresho kuanzia
kifungu Cha kwanza 1 hadi 38 ili kuwa na Sheria rafiki kwa tasnia ya habari nchini na kufanya kazi bila kikwazo.
Kwa upande wake afisa mawasiliano mkuu wa Umoja wa afrika AU, Wynne Musabayana amesema licha ya bara la Afrika kupiga hatua ya maendeleo katika tasnia ya habari lakini bado tunapaswa kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja ili kulinda haki za waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao vyema ya kuhabarisha umma.
Amesema wakati tukielekea kuadhimisha kilele Cha siku ya vyombo vya habari duniani, vyombo vya habari vya bara la Afrika vinapaswa kubadili taswira iliyowekwa kwamba bara la Afrika ni eneo la migogoro,rushwa na masikini na badala yake turipoti mambo ya maendeleo.
“Vyombo vya habari ni daraja na ufunguo wa maendeleo,amesema afisa mawasiliano mkuu wa Umoja wa Africa Wynne Musabayana”
Maadhimisho ya mwaka huu yanayofanyika katika Jiji la Arusha kwa bara la Africa yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Uwandishi wa habari na changamoto za zankidigiti”