Walemavu waomba kukumbukwa katika huduma muhimu

 * Wasema mikopo ya Halmashauri haiwatoshi na haitoki kwa wakati

*Watoa yao wakati wa kongamano la wiki ya Azaki Monduli

Na Seif Mangwangi,MONDULI

WATU wenye ulemavu wameomba kundi la watu wenye mahitaji maalumu kuendelea kukumbukwa katika jamii  Kwa kupatiwa huduma  muhimu kwa kuwa hawana uwezo wa kupata huduma hizo kwa kutumia nguvu zao.

Akizungumza jana wilayani Monduli,mkoani Arusha,wakati wa maadhimisho ya hafla ya wiki ya Azaki, kiongozi wa shirikisho la watu wenye ulemavu Monduli, Dora Msuya,amesema Kwa sasa kundi hilo,limekuwa halipewi kipaumbele kwenye baadhi ya mambo.

Mkurugenzi wa Foundation for civil society Wakili Francis Kiwanga  akiwa pamoja na maofisa wengine wa Azaki mbalimbali nchini wakipata maelezo kutoka kwa baadhi ya vikundi vilivyokuwa vikionyesha  bidhaa tofauti katika viwanja vya polisi Monduli

Aidha alisema mikopo ya asilimia mbili wanayokopesha na Halmashauri ni midogo na wakati mwingine inacheleweshwa,hivyo aliomba utaratibu wa kutoa fedha hizo uboreshwe ikaiwamo kuongeza kiwango cha ukopeshaji na kuwahishwa kutolewa.

Dora,ambaye ni kiongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Monduli,alisema pia kuna umuhimu mkubwa wakapewa msaada wa kupatiwa elimu kwa kuwa baadhi yao hawajasoma.

“Tunaomba kupewa fura ya elimu ya kawaida na ile ya ujasiria kwa kuwa baadhi yetu,hawakufanikiwa kusoma na hilo,likifanyika itasaidia kuongeza wigo wa kipato cha familia kutoka na kazi wanazofanya,”alisema.

Akijibu hoja hizo,Ofisa Maendeleo ya Jamii,Halmashauri ya Wilaya ya Monduli,Rose Mhina,alisema mpango wa ushirikishwaji wa makundi hayo,unaanzia katika mikutano ya vitongoji,vijiji na kata,lakini wako wananchi hawafahamu kinachoendelea katika maeneo yao kwa kuwa hawahudhurii kwenye mikutano hiyo.

Vilevile alisema suala la utoaji wa mikopo na urejeshaji una utaratibu wake,na wamekuwa wakiwajali ila vijana wamekuwa wakilegalega kurejesha hadi watumia vyombo vya dola ukilinganisha na wanawake ambao wamekuwa waaminifu.