Walioficha meno ya tembo wapewa mwezi mmoja wajisalimishe

Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia na kupata maelezo ya vipande 338 na
meno mazima ya Tembo 75 pamoja  na meno mawili ya kiboko yaliyokamatwa
kutoka kwa watuhumiwa 8 wa Ujangili na  Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya
Ujangili (NTAP). 
PICHA/Aron Msigwa – WMU
……………
Na. Aron Msigwa – WMU, Dar es Salaam.
SERIKALI imetoa muda wa mwezi
mmoja (kuanzia Septemba 4 hadi Oktoba 4, 2019) kwa wananchi wote
wanaomiliki meno ya Tembo kinyume cha sheria, kuhakikisha
wanayasalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba
watakaofanya hivyo kabla ya kuisha kwa muda huo hawatashtakiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa muda huo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa Habari jijini Dar es salaam mara baada Kikosi Kazi cha
Taifa dhidi ya Ujangili (NTAP) kukamata watuhumiwa 8 wa ujangili,
vipande 338 na meno mazima ya Tembo 75 pamoja  na meno mawili ya kiboko.
“Nimewaita hapa ili mshuhudie kazi
nzuri iliyofaywa na maafisa wa Serikali na Kikosi Kazi maalum cha
kudhibiti ujagili, ninatoa huruma ya mwezi mmoja kwa kila aliye na meno
ya Tembo ayasalimishe kwenye chombo chochote cha Serikali na
atakayefanya hivyo ndani ya muda huo hatutamshtaki” Amesisitiza
Dkt.Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla amesema kukamatwa
kwa majangili hao kumetokana na kazi ya muda mrefu ambayo imezaa
matunda na matokeo yake kuonekana kwa kukamatwa kwa majangili sugu 8
(nane) akiwemo Bw. Hassan shaban maarufu kwa jina la Nyoni aliyekuwa
akitafutwa kwa muda mrefu kwa kujihusisha na mtandao wa ukusanyaji wa
meno ya Tembo kutoka Tanzania na Msumbiji.
Amesema  mtuhumiwa huyo wa
ujangili amekamatwa na jumla ya vipande vya meno ya Tembo 338 na memo
mazima 75 pamoja pamoja na meno 2 ya Viboko ambapo kwa mujibu wa
Wataalam na Wanasayansi wa Uhifadhi wa Wanyamapori wanaeleza kuwa meno
hayo ni sawa na Tembo 117 waliouawa.
Amebainisha kuwa meno hayo
yalianza kutafutiwa soko mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ya
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilipoingia madarakani, hivyo hatua ya
Serikali kuimarisha  Ulinzi wa Rasilimali za Taifa  na kukiongezea uwezo
Kikosi cha Kudhibiti Ujangili soko la meno hayo liliharibika.
Dkt. Kigwangalla amesema katika
kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano Majangili wengi wamekamatwa na
mitandao yao kusambaratishwa akisisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na
biashara hiyo kwa namna yoyote ile atakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya Sheria.
“Mtuhumiwa huyu amehangaika na huu
mzigo kwa zaidi ya miaka minne na hili nataka watanzania wajue ya
kwamba yeyote atakayejihusisha na biashara hii ya kuuza nyara za
Serikali tutamkamata tu maana, sababu ni moja wateja tumebaki ni sisi
wenyewe popote utakapojaribu kuuza tutakukamata tu” 
Aidha, ametoa onyo kwa wananchi
wanaojihusisha au kushiriki kwa namna yoyote ile  na vitendo vya
ujangili waache mara moja akibainisha kuwa kazi hiyo kwa sasa haina
nafasi nchini Tanzania.
Amesema kuwa kuanzia mwaka huu
Wizara yake itaweka Mkakati mpya wa kukomesha vitendo vya ujangili
nchini hadi kufikia mwaka 2014 akieleza kwamba mkakati huo utaimarisha
kikosi kazi cha kudhibiti ujangili, kuimarisha ushirikiano na wizara
nyingine, kuimarisha Jeshi USU na kuweka muundo mzuri utakaozuia mauaji
ya wanyama.
Aidha, amefafanua kuwa katika
kipindi cha miaka 3 katika Ikolojia ya Selous hakuna Tembo hata mmoja
aliyeuawa na majangili akibainisha kuwa meno ya Tembo yaliyokamatwa
Agosti 31 mwaka huu ni yale ya ujangili uliofanyika nyuma kabla ya
kuingia kwa Serikali ya awamu ya tano.
Amesema Kikosi Kazi hicho cha
Serikali kimefanikiwa kuziba mianya yote ya biashara haramu za nyara za
Serikali kwa kupambana na uharifu kwa kufuatilia na kusambaratisha
mitandao yote ya ujangili ikiwemo mali na silaha za majangili.
Amebainisha kuwa kazi hiyo
imefanikiwa kwa kuwa kinajumuisha maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii na vyombo vingine vya ulinzi na Usalama  na taasisi za kisheria 
na kimekuwa kikifanya kazi nzuri ya kuratibu , kusimamia na kuchukua
hatua za kupambana na uhalifu wa rasilimali za Wanyamapori na Mazao ya
Misitu kwa kuendesha operesheni zinazoongozwa na taarifa za
Kiintelijensia.
Dkt. Kigwangalla ameongeza kuwa
Kikosi Kazi hicho kinafanya uchunguzi wa wahalifu na mali zinazotokana
na uhalifu, kukamata, kupekua na kushikilia mali za wahalifu
wanaojihusisha na ujangili.        
 “Sasa hivi kupitia Kikosi Kazi
chetu tumeziba mianya yote, anayefanya biashara tutamkamata, aanayewinda
kwenye maeneo ya hifadhi tutamkamata na hata askari wote
wanaoshirikiana na majangili tutawakamata kwa kuwa tukimpata jangili
mmoja tunahakikisha na mtandao wake wote tumeuvunja” Amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla ameeleza kuwa
katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 Kikosi Kazi hicho kimefanikiwa
kukamata watuhumiwa zaidi ya 1072 silaha 539 zikiwemo siala 85 za Kivita
na jumla ya risasi 37,921.
Aidha, nyara mbalimbali za
Serikali zilikamatwa ikiwa ni pamoja na meno tembo, pembe za faru, ngozi
za Simba, Chui na Duma, meno ya Kiboko, Kobe pamoja na mazao ya Misitu.
Pia Dkt. Kigwangalla amebainisha
kuwa Kikosi kazi hicho hadi sasa kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa
wakubwa wa ujangili wakiwemo Aloyce Francis Ayubu( Kamanda),  Mateso
Kassiani Albano (Mateso Chupi)  na Jayzan George Kuchar (China), Haruna
Kassa, Frank Silagei na Ojugu (Original).
Wengine ni Haong Nghia Trung, MS.
Yang Feng Glan (Queen of Ivory) ambaye amekwishahukumiwa pamoja na
Salvius Francis Matembo na Manase Julius Philemon, Boniface Maringo,
(shetani), Juma Maringo (Yesu), Godfrey James Nyamicha (Papa), Haidari
Omary Sharif, Oliva Lucas Mchua na Mrangilwa Emanueli.