Wananchi kijiji cha namijati wilayani nanyumbu watoa ya moyoni baada ya rais samia kuwapelekea mradi wa maji, wasema itakuwa mara ya kwanza kuona maji ya bombani

Baadhi ya mafundi wakiendelea na shughuli za ujenzi katika mradi mkubwa wa maji Kijiji cha Namijati utakaokwenda kunufaisha wananchi zaidi ya 3,800 katika Kijiji hicho na Kata ya Mkonona.RUWASA wanatekeleza mradi huo kupitia fedha za ustawi ambazo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Crila Bayo ambaye ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara (kushoto)akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa mradi huo.Kulia ni Mtangazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) Bertha Mwambela.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Crila Bayo akiwa amebeba bomba akimsaidia moja ya mafundi wanaoendelea na ujenzi wa tanki la maji ambalo linajengwa kijiji cha Namijati.
Sehemu ya mabomba yakiwa yamehifadhiwa kabla ya kutandikwa chini

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mkonona Dk.Peter Nangomo akimhudumia mwananchi wa kijiji hicho baada ya kupeleka ndoo ya maji katika zahanati hiyo.Kwa mujibu wa Dk. Nangomo wamekuwa na utaratibu wa mama mjazito anapokwenda kujifungua kwenda nan doo ya maji.


Mmoja ya wakazi wa Kijiji cha Namijati akiwa amebeba ndoo ya maji kichwani wakati akimpeleka mgonjwa wake kupata matibabu Zahanati ya Mkonona.

Ofisa Maendeleo ya Jamii-RUWASA Wilaya ya Nanyumbu akizungumza kuhusu umuhimu wa mradi huo wa maji.
Muonekana wa tanki la maji ambalo ujenzi wake bado unaendelea linavyoonekana kwa sasa.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Nanyumbu

MKAKATI wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtua Ndoo Mama kichwani umeendelea kutekelezwa kwa vitendo katika Wilaya ya Nanyumbu baada ya wananchi wa Kijiji cha Namijati ndani ya Wilaya hiyo kupelekewa mradi mkubwa wa maji ambao unatekelezwa kwa fedha za  Ustawi maarufu fedha za UVIKO-19. 

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa kufika kwa mradi huo mkubwa wa maji unakwenda kuwaondoa katika changamoto ya kutafuta maji umbali mrefu kiasi cha kukwamisha shughuli nyingine za maendeleo huku wakieleza kuwa itakuwa mara ya kwanza wananchi kushuhudia maji ya yakitoka bombani kwenye kijiji hicho.

Mkazi wa Kijiji cha Namijati Zubeda Hassan Bilali amesema yeye ni mzaliwa wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Mkonona na katika maisha yao yote wamekuwa changamoto ya uhaba wa maji kwa muda mrefu.

”Kuna wakati tunalazimika kutafuta maji mbali na kijiji chetu, tunakwenda kuchota maji hadi Ruvuma,hivyo kuja kwa mradi huu wa maji tunashukuru kwa mikono miwili na tunasema Rais Samia Suluhu Hassan ahsante.

Amefafanua katika kutafuta maji kuna wakati wanalazimika kulala mtoni na kurudi siku ya pili yake na hiyo imesababisha changamoto katika baadhi ya familia.”Mimi umri wangu ni miaka 50 na katika umri wote huo sijawahi kuona maji ya bomba hapa kwetu, lakini Serikali ya Awamu ya Sita imetambua changamoto yetu na leo tunaona mradi wa maji ambao utekelezaji wake unakwenda vizuri , hivyo tunakwenda kuondokana na adha ya maji.”

Kwa upande wake Ahmad Rashid Bakari ambaye naye ni mkazi wa Kijiji cha Namijati amesema wanatoa shukrani kwa Serikali pamoja na RUWASA Wilaya ya Nanyumbu kwa uamuzi wa kupeleka mradi wa maji kwenye kijiji hicho.”Tunajua ule mfumo wa kwenda kulala mtoni kwa ajili ya kufuata maji unakwenda kufika mwisho.”

Mkazi mwingine Abbas Yassin amesema uwepo wa mradi huo kwenye kijiji chao umenufaisha vijana wengi ambao wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za ujenzi , hivyo wanaishukuru RUWASA kwa kutekeleza mradi huo ambao ukikamilika unakwenda kunufaisha wananchi walio wengi.

”Tutatumia muda mwingi kufanya maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kwenye kutafuta maji.” Ameongeza wanampongeza Rais Samia Suluhu kwa kuwaona wananchi wa kijiji cha Namijati na kwamba walikuwa wanasikia tu Rais Samia anaupiga mwingi lakini kupitia mradi wa maji ulioko katika eneo lao wamethibitisha hilo na kweli anaupiga mwingi katika kuwatumia Watanzania.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kijiji cha Namijati Ally Mussa amesema anashukuru kufika maji kwenye kijiki chao, hivyo kwa hatua ambayo Serikali wamefikia wanashukuru, hivyo ombi lao kubwa ni kuona mradi huo unakamilika na utanufaisha kaya zaidi ya 600.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii-RUWASA Wilaya ya Nanyumbu Dariana Mbata amesema wakiwa kama wasimamizi wa huduma ya maj kwa wananchi wanaishukuru Serikali chini ya Rais samia kwa kuwapelekea huduma ya maji wananchi wa Namijati kwasababu kulikuwa na shida kubwa ya maji ambayo inakwenda kuondoka.

“Kukosekana kwa maji kumekuwa na changamoto kubwa hata kwa wajawazito ambao wanapokwenda kujifungua wanatakiwa kubeba na ndoo ya maji lakini baada ya mradi huu sasa maji sasa yatapatikana kwenye Zahanati, hivyo kutaondoa wajawazito kwenda na maji. Kwa hiyo hii huduma ya maji inakwenda kukomboa kizazi cha sasa na kijacho”.

Hata hivyo amewaomba wananchi wa Mitumbati na Namijati ambao ndio wanufaika wa mradi huu waendelee kutunza miundombinu ya maji ambayo Serikali imewekeza Sh.bilioni 1.3, lakini ni vema wakatambua mapema huduma ya maji itakuwa inachangiwa ili iwe endelevu.

Aidha Mkazi mwingine wa kijiji cha Namijati Bibiana Mnape amesema imekuwa kawaida yao wanapompeleka mama mjamzito kujifungua kwenye zahanati yao kwenda na ndoo ya maji na hiyo inatokana na changamoto ya muda mrefu ya kukosena kwa maji.

Kwa upande wake Mhanga Mfawidhi wa Zahanati ya Mkonona Dk.Peter Nangomo amesema wamekuwa na changamoto ya uhaba wa maji, hivyo imekuwa ni kawaida katika Zahanati yao wanawake wajawazito kwenda na maji.”Kuja kwa mradi huu tunaokwenda kuondoa hii changamoto ya wajawazito kuja na maji pindi wanapohitaji huduma.”

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) wilayani Nanyumbu Crila Bayo amefafanua mradi huo wa maji unaitwa mradi wa maji Mitumbatu chilinda, ambao unatekelezwa kata ya mkonona.

“Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 1.3, baada ya kukamilika utanufaisha wakazi zaidi ya 3,800 , katika kijiji cha Namijat na Mitumbati.Chanzo cha maji kinachotumika katika mradi huu ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 15,800 kwa saa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 50 na kazi mbalimbali za ujenzi zinaendelea” .