Wanawake wafunzwe teknolojia za kilimo

 

Na Doreen Aloyce, Dodoma. 

Serikali imetakiwa kuwawezesha wanawake hususani kwenye kilimo kwa kuwapatia teknolojia za kisasa za kilimo mbalimbali zinazoweza kupunguza athari ya mabadiliko ya Hali ya hewa na kusaidia kuinua kipato chao na Taifa kwa ujumla. 

 Hayo yameelezwa Jana  jijini Dodoma na Dr. Mkupete Jaah, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Campus ya Mkwawa Idara ya uchumi wakati alipokuwa Kwenye mkutano na wadau wa kilimo waliokiwa wakiwasilisha tafiti zilizofanywa juu ya Athari za hali ya hewa kwenye kilimo na jinsi gani ya kukabiliana nazo. 

 Kwa mujibu wa Dkt Jaah, tafiti hiyo imeonesha kwamba upatikanaji na utumiaji wa techolojia za kilimo zina uwezo mkubwa wa kupunguza tofauti ya kipato kati ya wanawake na wanaume wanaojihusisha na kilimo. 
 Dkt Jaah amesema hatua hiyo ni baada ya kufanya utafiti uliofanyika kuanzia mwaka jana januari 2022 mpaka Disemba ambao ulibaini wanawake wengi wanaojihusisha na kilimo wana changamoto ya vitendea kazi kutokana na vipato tofauti na wanaume. 

 Amesema kuwa Utafiti umeonesha kwamba wanawake wakitumia teknolojia hizo ikiwemo mbolea na vifaa ,wanafanikiwa zaidi kuliko mashamba ya wanaume lakini wasipotumia hizo teknolojia wanaume uwa na kipato kikubwa asilimia 24.
 Serikali ikiwekeza kwa wanawake watanufaika kuwasomesha watoto wao na kuwapa lishe bora ambayo itasaidia kuondoa udumavu kwa watoto ,kuondoa umasikini , kutunza familia na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii inayowazunguka .
 “Ni vyema serikali iangalie namna ya kuwasaidia wanawake kuwapatia Ruzuku kununua mbolea ambayo itawasaidia kulima na kupata mazao bora hii itawasaidia kujikomboa kiuchumi.” 
 “Lakini pia utafiti wetu umebaini wanawake wengi hawapati mikopo ya kuendesha kilimo tofauti na wanaume jambo ambalo wengi wamekuwa hawavuni mazao ya kutosha. 
Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya kisera kutoka Wizara ya Kilimo , Monica Kanawala amesema kuwa utafiti uliowasilishwa utaleta tija kwa serikali kwani umebainisha changamoto ambazo zinamuumiza mwanamke tofauti na mwanaume. 
 Amesema kuwa Serikali kupitia sera zake ikiwa ni sera ya Taifa ya kilimo ya mwaka 2013 pamoja na mikakati iliyopo inaendelea kutoa jitihada za kuwezesha upatikanaji wa pembejeo, zana za kilimo na teknolojia za kisasa ambazo zinamuwezesha mwanamke kuweza kishiriki kwenye kilimo pasipo kuumizwa.
 “Lakini pia serikali yetu inaendelea kutoa mbolea kwa Ruzuku kwa ajili ya kumsaidia mkulina na upatikanaji wa mbegu bora ambazo zitamsaidia mkulima anufaike na kilimo, “.
Kwa upande wake mdau wa sekta binafsi na mkulima Idd Senge amesema utafiti huo utasaidia kuwainua wakulima na kuongeza uelewa wa matumizi ya teknlojia hasa kilimo biashara ambao bado ni mdogo sana kwa jamii nzima wakiwemo wanawake.
Kuwa licha ya serikali kuweka mikakati ya kuwasaidia wanawake inapaswa itafute mbolea ambayo haitaleta madhara kwenye ardhi kwani wakulima wengi wanaogopa kutumia mbolea za viwandani kwa madai yanaharibu ardhi na inawalazimu kuitumia kila mwaka ambayo upelekea wenye vipato duni kushindwa.
 “Ni kweli tunashauri Kuwa serikali iwekeze kwa wanawake kuwapatia teknojia za kisasa lakini kuna haja ya kutoa elimu kwa jamii nzima ili kuondoa wimbi la umasikini kutokana na uwezo wa kupata mahitaji hasa kununua vifaa.”amesema Senge 
“Niiombe serikali isipuuzie huu utafiti kutoka kwa wataalamu wa chuo kikuu cha Dar es salaam, serikali iwasaidie wakulima kiujumla kuwapatia mbolea ambayo haina madhara ambayo itasaidia kutunza mashamba kwa kipindi kirefu itasaidia hata wanawake kuitumia vyema,”Amesema.