Na Mwandishi Wetu, APC BLOG Karagwe
WANUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Karagwe Mkoani Kagera, wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwapunguzia kero ya umaskini kupitia Mpango huo unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa katika vijiji vya Rulalo na Rukole, wanufaika hao wamesema Mpango huo umewawezesha kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa sana.
Wamesema mkakati wa Serikali wa kupambana na umaskini kupitia TASAF umeamsha ari ya kujiletea maendeleo na kuwawezesha kutunza kaya zao kwa uhakika tofauti na ilivyokuwa kabla ya uwepo wa Mpango huo.
“Hivi sasa na sisi tunaonekana watu, kwani tunaweza kujikimu na kupanga namna ya kuendesha maisha yetu kwa uhakika, tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kutujali’’. Amesema mmoja wa Walengwa katika kijiji cha Rukole, Rhoida Ernest.
Dkt. Mwanjelwa amesema kinachofanywa na Serikali kupitia TASAF ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mwenyezi Mungu ambayo hata katika Vitabu Vitakatifu vinazungumzia suala la kuwajali wasiojiweza ikiwa ni pamoja na yatima, wajane na maskini huku akinukuu Kitabu cha Yakobo: 1:27.
Dkt Mwanjelwa ameshuhudia namna Walengwa wa TASAF walivyoanzisha miradi mbalimbali ya kujiongezea kipato ikiwemo ufugaji wa mbuzi, kuku, ujenzi wa visima vya kuvuna maji ya mvua na uboreshaji wa makazi kwa kujenga nyumba na kuwa na uwezo wa kusomesha watoto ambao mahudhurio yamekuwa bora ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuingizwa kwenye Mpango.
Amewasisitizia wanufaika hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuondokana na umaskini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa amewaagiza watendaji wa Serikali kuwa karibu na walengwa wa TASAF ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati, lengo likiwa ni kuwawezesha kujiongezea kipato na kutekeleza shughuli zao za kiuchumi kwa tija zaidi.
Ameongeza kuwa, matokeo chanya yaliyoanza kuonekana kwa Walengwa wa TASAF yanapaswa kupewa msukumo na wataalamu hususani wa sekta za kilimo, ufugaji na uanzishwaji wa miradi ya kiuchumi ambayo itaboresha maisha yao.
Dkt. Mwanjelwa atahitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Kagera kwa kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi ambako atakutana na wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.