Kaimu mkurugenzi wa wizara ya mifugo Dkt Muhina akiteta baada ya kutembelea Banda la asasi ambao ndio wazamini wakuu katika mkutano wa 45 wa wana sayansi ya mifugo pamoja na uvuvi |
Na Queen Lema Arusha
Serikali imewataka watafiti kuendelea kufanya utafiti wa kisayansi kwenye sekta ya mifugo na uvuvi ambao utaleta mabadiliko katika sekta hiyo ambayo bado inaitaji watafiti wa kutosha
Pia watafiti wa masuala ya kisayansi ambao wameshafanya tafiti wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanawasilisha tafiti hizo kwa mamlaka husika kama vile halmashauri
Hayo yameelezwa mapema jana na kaimu katibu mkuu wizara ya mifugo na uvuvi Dkt Charls Muhina wakati akifunga mkutano wa 45 wa chama Cha wanataaluma wa sayansi ya mifugo pamoja na uvuvi (Tp)
Dkt Muhina alisema kuwa ili sekta hiyo iweze kuendelea mbele ni lazima kuwepo na watafiti wa kisayansi ambao watafanya kazi zao kwa uzalendo mkubwa sana na kuleta majawabu ya changamoto ambazo zinawakabili wadau wa sekta ya mifugo pamoja na uvuvi
Alidai kuwa kupitia tafiti ambazo wanazifanya wataweza kutatua changamoto pamoja na majanga mbalimbali ambayo yanatolewa kama vile majanga ya mabadiliko ya tabia ya nchi,Corona, ambayo yote hayo yamechangia kwa kiwango kikubwa sana kuwaangusha na kuharibu malengo ya katika sekta hiyo
“Si vibaya kama tukijifunza kwa nchi ambazo zimeendelea ambazo wao hata kama majanga yatatokea wafugaji na wadau katika sekta ya nyama hawayumbi wanabaki vile vile tujiulize wale wanatumia mbinu Gani ambayo ni mbadala na sisi tutumie hapo tutakuwa tumeweza kupiga hatua kubwa sana”aliongeza
Awali mwenyekiti wa chama hicho Dkt Jonasi Kizima alisema kuwa huo ni mkutano wao mkuu na wataweza kujadili mada 27 ambazo zote zinalenga kuimarisha maslai ya Taifa
“Tupo hapa Arusha tunalenga kuhakikisha kuwa tunajadili na tutakuja na majawabu juu ya mambo mbalimbali hasa ya kwenye sekta yetu kwa kuwa tunaamini kuwa sisi tuna mchango mkubwa”aliongeza
Akiongelea suala la utafiti alisema kuwa ni muhimu Sasa kwa kila mwana sayansi kuhakikisha kuwa kila tafiti ambazo wanazifanya ziweze kuwafikia wadau ili ziweze kuzaa matunda.
Naye Bw Joseph Joakimu kutoka katika kampuni ya Trouw Nutrition alisema kuwa mkutano huo utaweza kuboresha mambo mbalimbali ambayo yanaikabili sekta ya mifugo
Bw Joseph alisema kuwa yeye kama mdau wa mifugo wanaungana na watafiti wote kwa kusema kuwa ni muhimu tafiti ambazo zitafanyika ziweze kuzaa matunda
Alihitimisha kwa kusema kuwa kampuni ya Trouw Nutrition imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu na mbinu mbadala wafugaji waweze kuvuna mazao yenye faida kubwa .