Watakaofiwa na wazazi st anne marie kuendelea kusoma bure

Na Mwandishi Wetu 

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Dk. Jasson Rweikiza, amesema mwanafunzi ambaye atafiwa na wazazi wake wakati akiendelea na masomo kwenye shule yake ya St Anne Marie Academy hatafukuzwa shule kwa sababu ya kukosa ada. 

 Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza kwenye mahafali ya 20 kwa wanafunzi wa shule ya awali yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo, Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.

Alisema wakati wa mlipuko wa ugonjwa Corona wazazi 46 wenye wanafunzi kwenye mtandao wa shule hizo walikufa kwa ugonjwa huo lakini hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyefukuzwa shule mpaka sasa kwa kukosa ada. 

 “Nilisema wakati ule tulipopoteza wazazi 46 wakati wa Corona kwamba shule za St Anne Marie Academy hakuna mwanafunzi atakayefukuzwa baada ya mzazi wake kufa na kushindwa kulipa ada napenda kurudia na kusisitiza msimamo ni ule ule,” alisema na kuongeza

“Hata baada ya Corona vifo vipo na hakuna ajuaye kesho yake kwa hiyo hatufukuzi mtu hapa na kama mwanafunzi alikuwa shule ya msingi atamaliza darasa la saba bila kulipa ada na kama yuko sekondari atamaliza kidato cha nne bila kulipa ada,” alisema Dk. Rweikiza 

 Aidha, alisema siri ya mafanikio ya shule hiyo kitaaluma kila mwaka ni shule kuwa na mazingira mazuri ya wanafunzi kusomea ikiwemo maktaba ya kisasa na maabara iliyosheheni vifaa vya kutosha pamoja na na walimu mahiri wenye kujua kazi yao.

Alisema wanafunzi wa bweni wamekuwa wakila milo mitano kwa siku wakati wale wa kutwa hupatiwa milo miwili hali ambayo imechangia utulivu wa wanafunzi na kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa. 

 “Ninapozungumzia umahiri wa wanafunzi wa St Anne Marie wote mmeshuhudia namna mwanafunzi wa shule alivyomudu kusoma hotuba ya kurasa nne kwa kingereza bila shida yoyote, hiyo ni kazi kubwa ya walimu hongereni sana,” alisema 
Alisema shule imejitahidi kuweka miundombinu ya kisasa ya usalama wakiwemo walinzi 46 na mbwa wenye mafunzo kuwahakikishia wanafunzi usalama wanapokuwa shuleni hapo.

“Hawa askari 46 tulio nao wamepata mafunzo ya kisasa kiasi kwamba hata ukitokea moto wako tayari kuuzima ndani ya dakika chache sana kwa hiyo wazazi msiwe na wasiwasi na watoto wenu kitaaluma na kiusalama hapa St Anne Marie Academy,” alisema 

 Kwa upande wake, mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba, alimpongeza Dk. Rweikiza kutokana na mchango anaoutoa kwenye sekta ya elimu nchini.

“Kuhusu ubora wa elimu sina wasiwasi na nyinyi kwasababu nimemaliza kidato cha nne hapa mwaka 2005 shule hii naijua. Nakumbuka tulivyolelewa kwa maadili ya hali ya juu na kuhimizwa kusali kila mara na miundombinu niliyoikuta imenishangaza sana mmepiga hatua kubwa hongera sana Dk. Rweikiza,” alisema 

 Aidha, aliwataka wazazi kuwalea watoto wao kwenye maadili ya dini kwa kuwakumbusha kusali kila wakati badala ya kuwaachia walimu pekee jukumu hilo. 
 Aliwataka wazazi ambao watoto wao wamemaliza shule ya awali kuwaacha watoto wao wasome shuleni hapo kutokana na uhakika uliopo kuhusu maadili na kufanya vyema kwenye taaluma.

“Sote tunajua huko majumbani maadili yameporomoka sana kwa hiyo wazazi wamepekeni watoto kwenye shule ambazo mnauhakika watakuwa salama kimaadili na watafanya vyema kitaaluma,” alisema

Wanafunzi wa darasa la tatu shule ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakicheza wimbo wa akatambala ulioimbwa na msanii Saida Kalori, wakati wa mahafali ya 20 ya shule ya awali ya shule hiyo mwishoni mwa wiki.
Mbunge wa Viti Maalum, (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba akimlisha keki mmoja wa wahitimu wa shule ya awali ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, mahafali yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki. Anayeangalia ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza
  Mbunge wa Bukoba Vijijini, (CCM), Dk Jasson Rweikiza akimlisha keki mmoja wa wanafunzi wanaohitimu elimu ya awali ya St Anne Marie Academy, wakati wa mahafali ya 20 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga (CCM), Santiel Kirumba na kulia ni Mkuu wa shule hiyo, Gladius Ndyetabura.