Na Mwandishi Wetu
Wadau wa Sekta ya Asasi za Kiraia/Watetezi wa Haki za Binadamu tunapenda kutoa salamu za
pole kwa Rais wetu, Mhe Rais Samia Suluhu kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Aidha, kwa pamoja tumeendelea
kuungana na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
pamoja, viongozi wengine wa serikali na watanzania wote kwa ujumla katika kuomboleza kifo
cha Hayati Rais Magufuli. Wakati huo huo tunapenda kutumia fursa hii kumpongeza Mhe. Samia
Suluhu kwa kupata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchango wa Hayati Rais Magufuli katika Maendeleo
Wadau wa Sekta ya Asasi za Kiraia kwa ujumla tutamkumbuka Hayati Rais Magufuli kwa jitihada
kubwa alizozifanya katika kuleta maendeleo, kupiga vita rushwa, na ufisadi, kuboresha miundo
mbinu, kuboresha huduma za jamii, kuweka nidhamu ya utumishi wa umma nk. Tunatambua
kuwa tangu mwaka 1995 alipochaguliwa kuwa Mbunge na baadae kuteuliwa kuwa Naibu Waziri,
Waziri katika Wizara tofauti na baadae katika nafasi ya Rais, Hayati Rais Magufuli alikua mstari
wa mbele katika kupinga rushwa na kuleta uwajibikaji katika idara za umma. Aidha Hayati Mh.
Rais Magufuli alijitahidi kwa kiasi kikubwa kupigana vita dhidi ya umasikini na kuboresha miundo
mbinu.
Tunatambua kuwa, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kulikua na kilio kikubwa cha wadau
wa Asasi za Kiraia kuhusu mambo kadhaa ikiwemo kukosekana kwa uadilifu katika sekta ya
umma, utawala wa sheria, katiba mpya, haki za binadamu, umaskini miongoni mwa jamii,
changamoto katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu na nishati.
Hayati Rais Magufuli alijitahidi sana kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hizi pamoja na
kwamba zipo changamoto ambazo zilikuwa zinaendelea kufanyiwa kazi hadi umauti una mkuta.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali ikiwemo Ilani za Uchaguzi ya Asasi za Kiraia, yafuatayo ni
baadhi ya mambo muhimu yaliyofanyika au kukamilika katika kipindi cha uongozi wake katika
kukuza uchumi wa kitaifa.
(i) Kuendelea kuboresha utoaji na upatikanaji wa elimu kwa watoto. Utoaji wa elimu bure
katika ngazi ya Elimumsingi ni hatua ya kupongezwa.
(ii) Kuongezeka kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi
8,446 mwaka 2020;
(iii)Kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea
huduma za afya kutoka asilimia 42 ya mahitaji mwaka 2015 hadi asilimia 94.5 mwaka
2020;
(iv)Kukua kwa wastani wa pato la mwananchi kutoka shilingi 1,968,965 mwaka 2015 hadi
shilingi 2,458,496 mwaka 2018, na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia
6.9 kwa mwaka.
(v) Kuboresha miundo mbinu ikiwemo miundombinu ya nishati kama vile umeme wa mto
Rufiji, barabara, reli, viwanja vya ndege na bandari. Haya yamefanyika kwa lengo la
kurahisisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi kufanyika kwa urahisi na haraka.
(vi) Kuimarisha biashara kwa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga, mama lishe) kwa
kuwaongezea unafuu wa kulipa ushuru wa Shilingi elfu 20 kila mwaka. Hali hii imechangia
pia kurasimisha biashara hizi na kuongeza usalama wao ukilinganisha na hapo awali
walipokuwa hawatambuliki na kunyanyasika sana.
(vii) Kufufua shirika la ndege la serikali (ATCL) kwa kununua ndege mpya kwa fedha
taslimu. Hii ni hatua muhimu ambayo itatanua wigo kwa Watanzania kufanya biashara nje
na ndani ya nchi pamoja na kupanua sekta ya utalii nchini.
(viii) Kudhibiti mianya mingi ya wizi na utoroshwaji wa mali na rasilimali za taifa kama
vile madini. Jambo hili limepelekea ongezeko la pato la ndani la taifa. Kwa mfano katika
kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka 2018/2019 (Julai – Novemba), makusanyo
ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yalifikia TZS 7.37 trlioni sawa na 88.9%
ya makadirio ya TZS 8.30 trilioni katika kipindi hicho. Mapato yameendelea kukua mwaka
hadi mwaka kutokana na hatua stahiki zilizochukuliwa.
(ix)Kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi – kutokana na kuimarishwa kwa ufuatiliaji
kwenye taasisi, mashirika na kampuni kulikoiwezesha serikali kupata michango na gawio
stahiki kutoka kwenye uwekezaji wake.
(x) Kuimarika kwa matumizi ya technolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye wizara na
idara zinazojitegemea kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato uitwao
‘Government Electronic Payment Gateway’ (GePG) ambapo kati ya Julai 2017 hadi
Novemba 2018, jumla ya Taasisi za Serikali 325 zinatumia mfumo huu kukusanya
maduhuli.
(xi)Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, kumekua na uongezeko la upatikanaji wa umeme
kutoka megawati (MW) 1,308 mwaka 2015 hadi megawati (MW) 1,602.32 mwaka 2020.
Pia, usambazaji wa umeme vijijini umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 16.4
mwaka 2015 hadi asilimia 67.1 mwaka 2020;
(xii) Kuimarisha juhudi za kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, watoto
na wazee. Kutunga Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 ilikua ni moja ya hatua
kubwa kuhakikisha Serikali, Asasi za Kiraia na wadau mbalimbali wa haki za binadamu
wanachangia katika kulinda na kutetea haki za binadamu.
(xiii) Uwepo wa utayari miongoni mwa wizara na idara mbalimbali za serikali kukutana
na wadau wa Sekta ya AZAKI na kushirikiana nao kupunguza changamoto mbalimbali.
Moja ya mikutano muhimu ni mkutano wa Januari 2021 uliokutanisha wadau wa AZAKI
na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao uliibua mambo
mengi ya kufanyiwa kazi. Mikutano ya kila mwaka ya Wakurugenzi wa Azaki ambapo
wageni rasmi wamekuwa ni Mawaziri. Mikutano mbalimbali ya Azaki kufunguliwa na
Viongozi wa Serikali nk.
Haya ni baadhi ya mambo muhimu yatakayokumbukwa na wadau wa sekta ya Asasi za Kiraia
nchini. Haya mambo aliyoyatekeleza Hayati Rais Magufuli yanahitaji kusimamiwa na kulindwa
kwa umakini ili tusirudi tulipotoka. AZAKI tupo tayari kusaidiana na Mhe Rais Samia Suluhu
Hassan kuendeleza mazuri aliyosimamia Hayati Rais Magufuli. Kwa pamoja tunamwomba
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Hayati Mhe. John Pombe Magufuli mahali pema peponi, Amina.
Amemaliza kazi yake nzuri na ameatuchia sisi viongozi wenzake jukumu la kuyaendeleza.
Pongezi kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
Kufuatia kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi
wadau wa sekta ya Asasi za Kiraia tunapenda kutoa pongezi zetu za dhati kwa Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan. Tuna Imani kubwa naye kwa utendaji kazi uliotukuka katika kipindi chote cha
uongozi wake katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika huko nyuma.
Itakumbukwa kuwa Mh. Rais Samia amekua mdau mkubwa wa sekta ya Asasi za Kiraia. Kabla
ya kuingia kwenye siasa aliwahi kufanya kazi kwenye shirika la Association of Non-Governmental
Organizations in Zanzibar (ANGOZA) pamoja na World Vision. Na baada ya kuingia katika nafasi
za juu serikalini, mara kadhaa amekua mstari wa mbele kushiriki katika makongamano na
mikutano mbalimbali ya Asasi za Kiraia na taasisi za kiserikali. Haya yote ni baadhi tu ya mambo
yanayoendelea kutupa imani kubwa katika nafasi yake mpya kama Rais wetu na kwamba yeye ni
mmoja wa viongozi wanaoijua vyema sekta hii ya Asasi za Kiraia.
Mnamo mwaka 2014 wakati wa mchakato wa kuandaa mapendekezo ya Katiba Mpya, Mhe. Rais
Samia, akiwa Naibu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba alikua mstari wa mbele kuongoza
majadiliano kati ya wananchi, wabunge wa Bunge la Katiba na wadau mbalimbali ili tuweze
kupata Katiba bora ambapo mara kadhaa alishiriki mikutano mbalimbali ikiwemo ile iliyoandaliwa
na wadau wa sekta ya Asasi za Kiraia.
Katika nafasi mbalimbali alizoshika Mhe. Rais Samia amekua pia mstari wa mbele kufanya kazi
na wadau wa Asasi za Kiraia katika kuhakikisha mambo mbalimbali muhimu kwa jamii
yanatekelezwa. Miongoni mwa maeneo muhimu aliyosimamia moja kwa moja ni pamoja na
uboreshaji wa vituo vya afya na huduma ya afya, huduma ya maji (maarufu kama kampeni ya
‘kumtua mama ndoo’), kuboresha hali ya lishe kwa wakina mama wajawazito, watoto chini ya
umri wa miaka mitano, vijana balehe, na wazee, na kuzindua mradi wa kutokomeza unyanyasaji
wa wanawake na watoto masokoni. Pia amekua amekua akipambania kumuinua mwanamke
kiuchumi pamoja na kuwa mlezi wa mabaraza ya kumuinua mwanamke kiuchumi.
Mwaka 2016, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe Ban Ki Moon alitangaza kuanzishwa kwa
Jopo Kuu la Masuala ya Uwezeshwaji Wanawake Kiuchumi lilikuwa na jukumu la kuhamasisha
hatua madhubuti za kuchukua katika kuleta usawa wa kijinsia, kutoa mapendekezo mahsusi ya
utekelezaji wa malengo endevelu na hasa lengo namba 5 (kufikia usawa wa kijinsia; kuwawezesha
wasichana na watoto) na lengo namba 8 (kuinua mustakabali wa kukuza uchumi na kuhakikisha
ajira stahiki za kudumu). Aidha, Katibu Mkuu Mhe Ban Ki Moon alimteua Mhe Rais Samia akiwa
Makamu wa Rais kuwa Mjumbe wa Jopo Kuu la Viongozi wa Dunia kama Mwakilishi wa Nchi
za Afrika hivyo Mhe Rais wetu, Mhe Rais Samia anaouelewa mpana sana wa masuala haya
ambayo ndio kilio cha watoto, vijana na wanawake nchini.
Si hivyo tu. Mhe. Rais Samia ameshiriki katika makongamano mengi yaliyoandaliwa na Asasi za
Kiraia kwa lengo la kujadili na kuboresha upatikanaji wa haki za makundi mbalimbali katika jamii
kama vile haki za Wanawake na watoto. Katika nafasi mbalimbali alizoshika na hata katika nafasi
yake ya Makamu wa Rais, amekua akishiriki katika makongamano mbalimbali, mfano
makongamano ya wanawake na makundi mengine katika jamii.
Miongoni mwa mikutano iliyoandaliwa na AZAKI aliyopata kuhudhuria ni pamoja na Ushiriki
wake wa karibuni kabisa mnamo Tarehe 8 Machi 2021, aliposhiriki katika Maandhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani mkutano ulioandaliwa na Asasi ya Mwanamke na Uongozi, na mkutano
wa Mwanamke na Uongozi ulioandaliwa na Chama cha Waajiri nchini (ATE) Machi 4, 2021.
Mikutano mingine aliyohudhuria ni pamoja na ifuatayo.Uzinduzi wa Mtandao wa Wanawake
Viongozi Bara la Africa mwaka 2020 (African Women Leaders Network-AWLN), Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake mwaka 2019 (Mtandao wa Wanawake na Katiba), Mkutano Mkuu wa
Wanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Nchini mwaka 2018 (Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania-TAWLA), Tamasha la 14 la Mtandao wa Kijinsia mwaka 2017 (TGNP),
Maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania mwaka 2017 (THRDC), na
Mkutano wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Wabunge wa Bunge la Katiba mwaka 2014
(THRDC); na mikutano mingine.
Katika kushiriki mikutano ya AZAKI na kutoa ushirikiano kwenye kazi mbalimbali
zinazoandaliwa na Asasi za Kiraia tunapata tumaini na nguvu kubwa ya kuimarisha utoaji huduma
mbalimbali kwa jamii kupitia Asasi za Kiraia. Yafuatayo ni baadhi ya maeneo ya muhimu ambayo
sisi Wadau wa sekta ya Asasi za Kiraia tunatarajia kuendelea kuboresha na kufanya kazi karibu
zaidi na serikali ili kuhakikisha tunachangia katika mafanikio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan:
(i) Kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi kwa fedha zinazotumika katika miradi
mbalimbali. Katika taarifa iliyotolewa na Asasi za Kiraia katika wiki ya Asasi za Kiraia
Novemba 7 mwaka 2019, mashirika 16 yaliyofanyiwa utafiti yalionyesha yameingiza
nchini shilingi bilioni 236 katika kipindi cha miaka mitatu tu (2016-2018) kwa ajili ya
kutelekeza miradi mbalimbali nchini.
(ii) Kuboresha utendaji kazi wa Asasi za Kiraia na hivyo kuongeza tija katika utoaji wa
huduma mbalimbali. Kwa mfano sisi wadau wa Asasi za Kiraia tutaendelea kusaidia katika
kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu za afya, elimu, maji na kadhalika.
(iii) Kuongeza miradi ya kibunifu na yenye tija kwa jamii na makundi mbalimbali kama vijana,
watu wenye ulemavu, wanawake, watoto na wazee.
(iv)Kuongeza uwezo wa kifikra na kiuchumi miongoni mwa wanajamii kupitia elimu na
miradi mbalimbali ya kujenga uwezo itakayofanywa na wadau wa Asasi za Kiraia
(v) Kuchangia ongezeko la utawala bora katika taasisi za kiserikali kutokana na ufuatiliaji
utakaoendelea kufanywa na Asasi za Kiraia na wadau mbalimbali wa utawala bora na haki
za binadamu.
(vi) Kuchangia kutokomeza umaskini nchini kupitia miradi mbalimbali ya AZAKI.
(vii) Kushirikiana na serikali kutoa huduma kwa maeneo mbalimbali
(viii) Kuweka mikakati na serikali ya namna ya kutoa ajira kwa maelfu ya vijana
Tanzania.
(ix) Kulinda Katiba, haki za binadamu na utawala bora
(x) Kutoa msaada wa kisheria kwa wasiokuwa na uwezo wa kuweka wakili
(xi) Kuendelea kuwa walipa kodi wazuri hapa nchini
(xii) Kufanya kazi zetu kwa uwazi na kwa weledi na kufuata miongozo ya serikali
(xiii) Kuishauri serikali katika mambo ya msingi yanayohusu usimamizi wa sekta ya
AZAKI hapa nchini ikiwemo kuweka mazingira wezeshi ili sekta ya Asasi za Kiraia kukua
na kustawi kama ambavyo Ilani ya CCM 2020-2025 ilivyoahidi
(xiv) Kumshauri Mhe Rais Pamoja na serikali kuendelea kusimamia utumishi wa umma
kwa ukakamavu mkubwa kwa mujibu wa taratibu na misingi iliyopo ya kisheria.
(xv) Kuendelea kuishauri maboresho ya sheria mbalimbali kandamizi ikiwemo namna
bora ya kuimarisha utawala bora
(xvi) Kuendelea kuvishauri Vyama vya Siasa kuweka utaratibu wa kupata na kutambua
uwakilishi Bungeni wa Asasi za Kiraia (ikijumuisha mashirika ambayo sio ya kiserikali –
NGOs) kama ambavyo Chama Cha Mapinduzi kilivyofanya na kuishauri Serikali kuwepo
utaratibu wa kisheria wa kuitambua nafasi hiyo
(xvii) Kuendelea kuishauri serikali na wadau mbalimbali kuhusu kuboresha usawa wa
kijinsia katika nafasi mbalimbali za uongozi.
(xviii) Kushauri viongozi, wadau mbalimbali na wananchi kuhusu mambo muhimu
yatakayoweza kuboresha Amani ya taifa letu kwa mujibu wa Katiba na Sheri za nchi yetu.
Ni imani yetu kuwa kutokana na kazi kubwa aliyofanya Mh. Rais Samia katika nafasi mbalimbali
alizoshika, ataendelea kutumia uzoefu wake na kwa kushirikiana na viongozi wengine walio chini
yake katika kuhakikisha kuwa taifa letu linaendelea katika mwelekeo mzuri wa kimaendeleo ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii. Sambamba na hayo, ni matumaini yetu kuwa kadiri ambavyo ratiba
yake itaruhusu, Mhe Rais Samia Suluhu Hassan atatupa fursa ya sisi kama wadau wa Asasi za
Kiraia kukutana nae ili kupata dira na mahitaji yake ya namna bora ya kuendeleza na kuimarisha
mashirikiano kati ya Asasi za Kiraia na idara mbalimbali za serikali.
Hongera Mh. Rais Samia Suluhu Hassan. Mungu akulinde na akuongoze.
Mungu Ibariki Tanzania.
Imetolewa leo tarehe 29 March, 2021