Watumishi hewa bado wapeta na vyeti feki tanzania

 Na Mwandishi Wetu, APC BLOG

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Wakuu wa Taasisi za Umma na Maafisa
Utumishi nchini kumaliza zoezi la uhakiki wa vyeti vya Watumishi wa Umma vya ufaulu wa kidato cha Nne, cha Sita na Ualimu  kwa kile alichodai ofisi yake
imekuwa ikipokea taarifa za uwepo wa watumishi wachache wenye vyeti vya kughushi katika baadhi ya halmashauri na taasisi za umma.

Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo ikiwa ni sehemu ya msisitizo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 2015 ambapo
alielekeza utumishi wa umma nchini uwe wa uadilifu, unaowajibika na wenye sifa stahiki.

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa uwepo wa taarifa za watumishi wenye vyeti vya kughusi mpaka sasa unaashiria kuwa kuna baadhi ya Wakuu wa
Taasisi na Maafisa Utumishi hawajalipa uzito unaostahili zoezi la kuwaondoa watumishi wenye vyeti vya kughushi.

“Mpaka sasa bado tunapata taarifa za baadhi ya watumishi wenye vyeti vya kughushi kuendelea na utumishi wa umma katika baadhi ya
halmashauri na taasisi, hivyo inatulazimu kuwasilisha vyeti vyao Baraza la Mitihani kwa ajili ya uhakiki badala ya kuendelea na utekelezaji wa
majukumu mengine ya kitaifa,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Sanjari na hilo, Dkt. Ndumbaro amewataka watumishi wa umma nchini kuwajibika kwa Serikali na wananchi pindi wanapofuata huduma katika
taasisi zao ili kujenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wananchi.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa Wakuu wa Taasisi kuhakikisha wanasimamia nidhamu mahala pa kazi ili watumishi wa umma waweze
kutumia muda wao wa kazi vizuri kwa kutoa huduma bora kwa umma.