Waziri mkuu amuhakikishia rais a.kusini ushirikiano wa kutosha


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Amesema Tanzania inahitaji uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususan katika kipindi hiki ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati..

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 16, 2019) wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro.

Ameyasema kwa kuwa changamoto zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali zinafanana kwa kiasi fulani na zile za Afrika Kusini kwani historia za nchi hiyo na jiografia vinafana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mazimbu, Waziri Mkuu amesema kuwa lina uhusiano mkubwa na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.

Waziri Mkuu amesema eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

“Mheshimiwa Rais, Tanzania ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele (Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”. 
                                                       
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sera za ubaguzi wa rangi zilikoma mwezi Februari 1994 na kufuatiwa na uchaguzi huru na wa haki uliopelekea kupatikana kwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Hayati Mzee Nelson Mandela mwezi Mei 1994.

“Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote tutawakumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyerere na Hayati Mzee Nelson Mandela kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya umoja katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”.

Amesema misingi imara iliyojengwa na wazee wetu hao, imekuwa chachu ya ushirikiano kwenye majukwaa ya Kimataifa hususani katika kupambana na ubaguzi wa kiuchumi na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema namna pekee ya kuwaenzi viongozi wetu hao ni kuendelea kujenga umoja na kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa ulioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.

Rais huyo wa Afrika Kusini amesema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Serikali Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza teknolojia.

Pia amesema watairisha chuo cha SUA kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ili kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa. “Tutaboresha na shule katika eneo hili na kuweka utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika Kusini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.”

Rais Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na Waziri Mkuu. Kisha alitembelea campus ya Solomon Mahlangu na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.

Pia kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo alitembelea campus ya Mazimbu na kujionea sehemu ambazo waliishi wapigania uhuru wa nchi yake na kisha aliweka shada la maua kwenye makaburi ya wapigania uhuru. Ameondoka uwanja wa ndege wa Morogoro na kuelekea jijini Dar es Salaam saa 1.59 mchana.