Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kutumia sheria na taratibu zilizopo kulinda Wanyama waliohifadhiwa katika hifadhi za taifa pamoja na mapori ya akiba hapa nchini.
Mhe. Waziri Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 07 Septemba, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanga Mhe. Joseph Anania Thadayo wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu ambapo alitaka kujua kuwa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inapitia upya sheria za uhifadhi ambazo ziliwekwa kwa ajili ya kulinda uhifadhi lakini poa sheria hizo ziwalinde wananchi hata ikibidi kujitoa kwenye baadhi ya mikataba ya kimataifa ambayo inatushurutisha kuweka sheria ambazo zinawadhuru wananchi na mali zao.
Akijibu swali hilo Mhe. Majaliwa alisema kwamba kumekuwa na taarifa mbalimbali zikieleza kuwa kumekuwa na usumbufu mkubwa wanaopata wananchi kutoka kwa Wanyama wakali na waharibifu hasa wale wanaoishi pembezoni na maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori.
Amesema kwamba kwa kutumia sheria zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kulinda wanyamapori pamoja na wananchi wanaozunguka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutumia sheria zilizopo.
Mhe Majaliwa amesema moja wapo ya mikakati wa serikali ni kuongeza askari wa uhifadhi kwa ajili kuimarisha wa doria kwenye maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na kudhibiti uwindaji haramu.
Vilevile, amesema Serikali kupitia wizara ya maliasili imekuwa ikitumia ndege kuwarudisha wanyampori kutoka kwenye maeneo ya wananchi ili warudi kwenye maeneo yao yaliyohifadhiwa.
Sambamba na hayo, Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa wizara ya Maliasili na Utalii imeunda tume kwa ajili ya kutathimini mahitaji ya namna gani serikali inaweza kubadilisha sheria za uhifadhi kwa ajili ya kuzipitia na kuzifanyia marekebisho pale itakapobidi.