Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amefanya Ziara ya Kikazi katika kampuni ya Mawasiliano ya Tigo na kujionea kampuni hiyo inavyofanya kazi.
Akizungumza baada ya Ziara hiyo Waziri Nape amezipongeza kampuni za Simu nchini kwa kuendelea kutoa huduma zinazochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya Mawasiliano nchini.
“Kampuni za Simu zimechangia sehemu kubwa katika maendeleo ya nchi yetu sababu wanalipa kodi, wanaajiri Watanzania wengi sana hasa vijana , lakini pia huduma zao zinasaidia huduma nyingine mfano ulipaji wa kodi, utumaji na upokeaji wa fedha na mambo mengine kadha wa kadha kwahiyo mchango wao ni Mkubwa Sana” Alisema Waziri Nape.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo CPA Innocent Rwetabura amemshukuru Waziri Nape kwa kufanya Ziara hiyo na kumuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuchangia pato la Taifa.
Amesema Tigo imekuwa ikijivunia kuendelea kutoa ajira nyingi kwa Watanzania kupitia huduma mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitoa kupitia katika kampuni hiyo.
” Sisi kama Tigo Tanzania ni Kampuni ambayo tumewekeza zaidi ya Dola Bilioni 1.5 toka tumeanza , na tunatarajia kuwekeza zaidi ya Milioni 500 kuanzia sasa hivi kwa miaka mitano ijayo ili kuweza kuboresha Mawasiliano na ubora wa huduma Tunazotoa , kwa kipindi cha mwaka jana tumeweza kulipa kodi ambayo inafikia kiasi cha Shilingi Bilioni 370 , pamoja na kuajiri zaidi ya watanzania 1,233 na Mawakala zaidi ya 2020,000,” Alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo CPA Innocent Rwetabura