Basata yamfutia usajili msanii dudubaya …sasa marufuku kujihusisha na sanaa

Msanii
wa muziki wa Bongo Flava nchini, Dudubaya amefutiwa usajili na baraza
la sanaa la Taifa (BASATA) ambapo  baraza hilo pia limetoa onyo kwa
taasisi, kampuni na mtu yeyote kutofanya kazi na msanii huyo. Hatua hiyo
imekuja baada ya msanii huyo kukataa wito wa baraza hilo.



Dudubaya
ambaye jina lake halisi ni Godfrey Tumaini alitakiwa kufika ofisi za
Basata leo Januari 7, 2020 saa 4:00 asubuhi baada ya kusambaa kwa video
zake kwenye mitandao ya kijamii akizungumzia mambo mbalimbali, ambapo
Basata imeeleza ametumia kauli zisizokuwa na maadili wala staha.



Hata hivyo, Dudubaya aliukataa wito huo kwa kulijibu baraza hilo
kuhangaikia kwanza na migogoro iliyopo kati ya baadhi ya vyombo vya
habari na wasanii ili kuufanya muziki usonge mbele huku maneno
aliyoyatumia katika video zake akieleza kuwa ni ya kawaida.
Kutokana na kutoitikia wito huo, Katibu Mtendaji, wa baraza hilo,
Godfrey Mngereza katika tamko lake hilo amesema baraza limechukua hatua
ya kumfutia usajili wake kuanzia leo Januari 7,2020.