Aua mpenzi wake baada ya kumkumbushia ahadi ya ndoa

Na Asna Kaniki, Mwananchi 

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la
Paschal (24), anadaiwa kumuua mpenzi wake, Rosemary Gallus (34) mkazi
wa Gongo la Mboto kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni na kisha
kujiua sababu ikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa polisi wilaya ya Ilala, Zuberi Chembela alisema tukio hilo
lilitokea Ijumaa iliyopita ambapo kijana huyo alikwenda nyumbani kwa
Rosemary kwa lengo la kumaliza tofauti zao baada ya kugombana.
“Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja na wamezaa mtoto ambaye ana mwaka
na miezi kadhaa, ugomvi wao ulianza baada ya binti kukumbushia kuhusu
ahadi yao ya ndoa, mwanaume alisita hivyo binti alianza kutomuamini na
ugomvi ukaanzia hapo,” alisema Chembela alipokuwa akizungumza jana kwa
njia ya simu.
Hata hivyo baada ya kijana huyo kusita kutoa msimamo wake kuhusu kufunga
ndoa binti aliamua kuondoka nyumbani alipokuwa akiishi na mzazi mwenzie
na kwenda kupanga Gongo la mboto.
Alisema kwa kuwa marehemu hao walikuwa wazazi, waliendelea kuwasiliana
na kijana huyo alipafahamu alipopanga mpenzi wake na hatimaye alikwenda
kwa ajili ya kuzungumza na kumaliza tofauti zao.
“Badala ya usuluhishi ikawa ugomvi tena huku mwanaume akimtuhumu
mwanamke kuwa anamsaliti kisha kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni
mara mbili na kisha yeye mwenyewe kujichoma kitu tumboni mara mbili.”
Alisema kwamba baada ya hapo majirani walisikia mtoto akilia ambapo siyo
kawaida yake ndipo walipokwenda kugonga hata hivyo hawakujibiwa, kwa
kuwa mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, ndipo baadaye walipoamua
kuuvunja mlango huo.
Kamanda Chembela alisema majirani hao walipofika ndani walimkuta mtoto pembeni ya maiti za wazazi wake huku akiwa analia.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Chembela amewataka wananchi kuacha
kujichukulia sheria mkononi kama alivyofanya kijana huyo ambapo alidai
kuwa ni kinyume cha sheria.

CHANZO – MWANANCHI