*Akunwa na harakati za APC dhidi ya utetezi wa Haki za Waandishi wa habari
Egidia Vedasto.
Balozi wa Sweden Nchini Tanzania, Charlotta Ozak Macias amedai kuridhishwa na namna ambavyo Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC) inavyotetea haki za waandishi wa habari mkoani humo na kuahidi kuendeleza ushirikiano kwa UTPC ambayo ndio mlezi wa klabu zote nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Katika ofisi za APC Jijini Arusha Jana, Balozi Charlotta amesema Nchi ya Sweden imekuwa ikiifadhili UTPC kwa zaidi ya miaka10 sasa ili kusaidia uratibu wa vilabu nchini kwa kuwapa mafunzo na kusaidia Maendeleo ya Klabu hizo.
Aidha amewataka Waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii, kuzitambua haki zao hususan katika uchaguzi ujao kwa maana ya kujiandikisha, kupiga kura na kumchagua wamtakaye.
“Kipekee nawapongeza Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha licha ya changamoto mnazopitia, bado mmekuwa mkifanya kazi kubwa kuibua habari za kijamii na za kitaifa kwa ujumla, lakini pia mmeweza kuwa na miradi mingi, hiyo ndio lengo letu,” amesema Balozi Charlotta.
Kwa upande wake Afisa miradi kutoka Ubalozi wa Sweden anayeshughulikia masuala ya elimu na haki katika jamii, Stephen Chimalo, amesema Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC), ni miongoni mwa vilabu vichache ya mfano nchini vyenye umoja, utawala bora na maendeleo yao binafsi.
Chimalo amesema, sapoti inayotolewa na Serikali ya Sweden kwa UTPC inasaidia waandishi kupata maarifa na kuinua uchumi wao kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia mwamvuli huo wa waandishi wa habari nchini.
“Nawakumbusha tu kuongeza juhudi katika kuandika habari zinazoigusa jamii na kuibua maudhui mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi, elimu, afya na mengine mengi” ameeleza Chimalo.
Mkurugenzi wa Umoja wa klabu za Waandishi wa Habari Nchini ( UTPC), Keneth Simbaya, amesema Ubalozi wa Sweden umekuwa msaada mkubwa kwa klabu za Waandishi wa habari nchini.
“Kila mmoja wenu ni shahidi na ameshanufaika na mafunzo yanayotolewa na UTPC, hii yote ni kwa sababu ya msaada ambao tumekuwa tukipewa na nchi hiyo na bila wao tusingekuwa na hatua hii kubwa” amesema Simbaya.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Mkoa wa Arusha Claud Gwandu, amesema nchi ya Sweden imekuwa na msaada mkubwa kwa Maendeleo ya Klabu za Waandishi wa habari nchini ikiwemo APC.
Amesema Maendeleo ambayo APC inajivunia nayo hivi sasa ni matunda ya msaada wa Serikali ya watu wa Sweden kupitia mfuko wake wa Maendeleo wa SIDA.
“Mchango wa UTPC kwetu ni mkubwa, ukianza na mafunzo, ushauri na kuwezeshwa katika masuala ya kulipa kodi ya ofisi, kuwezesha mikutano ya waandishi, hii yote shukrani zinarudi kwa Nchi ya Sweden” ameeleza Gwandu.
Mmoja wa Waandishi wa habari aliyehudhuria kikao hicho Bertha Ismail ametaja namna ambavyo amekuwa akifaidika kwa kuwa mwanachama wa APC, ni pamoja na kupata fursa za mafunzo na ushirikiano miongoni mwa wananchama wenzake.
“Ukiwa Mwanachama wa APC unapata faida nyingi sana ukiacha fursa za mafunzo ambazo zimekuwa zikitukiza kitaaluma, pia hiki chama kumekuwa kikituunganisha na kutufanya kuwa wamoja, niwakaribishe waandishi wengine wajiunge,”amesema.