Bohari ya dawa (msd) yapongezwa kwa usambazaji wa dawa nchini

 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (kushoto), akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI) katika ziara yake ya kikazi ya
kutembelea Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam kujua changamoto
walizonazo za upatikanaji wa dawa na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja
katika ziara iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es
Salaam.

 Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa
Ubongo Muhimbili (MOI), Respicious Lwezimula (kulia), akizungumza katika
kikao hicho.
 Mkurugenzi
Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (wa tatu kushoto),
akizungumza na viongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika ziara
hiyo.
Kikao kikiendelea.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (wa nne kulia), akiwa na viongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI)
 Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Amani Malima,
akizungumza na viongozi kutoka MSD. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Laurean Bwanakunu na Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Celestine
Haule.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa
(MSD), Laurean Bwanakunu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na
viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke baada ya kufanya nao
mazungumzo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Na Dotto Mwaibale

BOHARI ya Dawa (MSD), imepongezwa kwa kushinda tenda ya kununua dawa Jumuhiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

Pongezi hizo zimetolewa Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili(MNH), Profesa Lawrence Mseru wakati akizungumza na
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu na timu yake wakati wakiwa
katika ziara ya kikazi ya kutembelea Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam
kujua changamoto walizonazo za upatikanaji wa dawa na kuzitafutia
ufumbuzi wa pamoja.

“Kwanza tunawapongezeni MSD kwa
kufikia hatua ya kununua dawa katika Jumuhiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) hii ni hatua ya kujivunia kama nchi” alisema
Profesa Mseru.

Mseru aliongeza kuwa licha ya
kuwepo changamoto ndogo ndogo MSD imejitahidi katika huduma ya
usambazaji wa dawa hapa nchini hivyo akaomba ushirikiano baina yao
uendelee kudumishwa ili kutoa huduma nzuri zaidi ya kuwahudumia wananchi
ukizingatia kuwa taasisi hizo zote zinafanya kazi ya Serikali.

Akizungumza katika ziara hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na
Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI),Respicious Lwezimula alisema kazi
kubwa inayofanywa na MSD inapaswa kuungwa mkono kwa kununua dawa na
vifaa tiba.

“Tuna kila sababu ya kuwaunga
mkono hawa wenzetu kwa kununua vifaa tiba na dawa kutoka kwao badala ya
kununua kwenye maduka ya watu binafsi kikubwa tunawaomba bei yao iwe
tofauti kidogo” alisema Lwezimula.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Amani Malima alisema suala la manunuzi ya dawa
na vifaa tiba linachangamoto kubwa lakini MSD wamesaidia sana
kuzipunguza kutokana na ushirikiano wanaofanya baina yao na wateja wao
hawana budi kupongezwa.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean
Bwanakunu amewaomba wateja wao hao kufanya Maoteo ya mahitaji yao sahihi
na kuyawasilisha MSD kwa wakati kwa mujibu wa sheria yaani tarehe 30
Januari kila mwaka,hasa dawa na vifaa tiba vinavyonunuliwa kwa manunuzi
maalumu.

Bwanakunu alihimiza watoa huduma
katika hospitali hizo kutambua jukumu walilonalo katika usimamizi wa
matumizi ya dawa na vifaa tiba kwa wananchi.

Akizungumza katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Temeke na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya
Fahamu na Upasuaji wa Ubongo Muhimbili (MOI), Bwanakunu alisema
anazitambua changamoto zilizopo za usambaji wa dawa na vifaa tiba na
kuwa MSD katika kukabiliana na changamoto hizo imepata msaada wa magari
220 kutoka Global Fund ambayo yataboresha usambazaji kutoka mara nne kwa
mwaka hadi mara sita kwa mwaka.

Kuhusu vifaa vya Manunuzi maalumu
Bwanakunu amesema hospitali zikiwa zinaomba kwa wakati mmoja
ingerahisisha kuagiza vifaa hivyo mapema,badala ya kila hospitali kuleta
kwa wakati wake.

“Vifaa hivi tunaagiza nje ya nchi
na mchakato wake unachukua muda mrefu hivyo tukipata oda mapema
itatusaidia kupunguza changamoto hiyo ” alisema Bwanakunu.