Chadema mkoa wa shinyanga watuma ujumbe mzito baada ya kuzuiliwa mkutano wa hadhara, zimamoto wawajibu

 

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi, akionyesha majibu ya barua za zuio la kutumia uwanja wa Zimamoto uliopo Nguzonane mjini Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Shinyanga Mjini kimelalamikia kunyimwa eneo la kufanyia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Zimamoto Nguzonane Manispaa ya Shinyanga.

Hayo yamebainishwa na viongozi wa chama hicho leo Juni 8,2024 wakati wakizungumza na waandishi wa habari ambapo wamelilalamikia jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga kwa kuwanyima nafasi ili kufanya mkutano wao  wa hadhara katika uwanja wa jeshi hilo na kwamba  mara nyingi uwanja huo hutumika kwa ajili ya mikutano mbalimbali.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi, pamoja na mambo mengine amewasisitiza wananchi wote kujitokeza kwenye mkutano huo wa hadhara Jumatano Juni 12,2024 huku akieleza malengo ya mkutano huo wa hadhara.

“Tumeazimia wiki ijayo siku ya Jumatano tarehe 12,06,2024 tutafanya mkutano eneo hilo hilo watake au wasitake tumeona hili ni shambulio la demokrasia na sisi ni wadau namba moja chama kikubwa cha upinzani kiweze kuzuiliwa kufanya mikutano kwa sababu ambazo hazina miguu wala kichwa, tumeanziamia na tunawaomba wananchi na watanzania watuelewe na wajitokeze kwa wingi siku ya Jumatano tarehe 12 tutafanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye eneo hilo hilo ambalo wanataka kutuzuia tumejiridhisha sababu walizozitoa hazina mantiki wala hazina kitu chochote cha kisheria”.

“Lengo na madhumini ya mkutano wetu huu ni kutoa elimu ya uraia tunapoelekeza kwenda kuandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lazima tutoe elimu ya uraia wananchi waweze au wapenzi wa CHADEMA waende wakajiandikishe lakini jambo la pili ni maandalizi ya serikali za mitaa mtakumbuka mwaka huu tunaenda kuchagua viongozi katika serikali za mitaa”.amesema Mhe. Ntobi

“Ukiangalia Barua hizi Mbili za Zimamoto zina Majibu Tofauti, hapa inaonyesha kuna kitu au wamepokea maelekezo kutoka Juu, hata Tundu Lissu tumeshuhudia amekuwa wakinyiwa Viwanja vya kufanya Mikutano ya hadhara kwenye baadhi ya Mikioa, ina wezekana kuna Mikakati inatengezwa chini kwa chini,”.

“Mbona Mwaka jana tulifanya Mkutano wa hadhara kwenye Viwanja hivyo, kwa nini sasa hivi tuzuiwe hasa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikaliza Mitaa, hivyo basi pamoja na mazuio yao sisi siku hiyo ya Jumatano ambayo ni Juni 12 tutafanya Mkutano hapo watake wasitake sababu zao hazina Mantiki wala Kisheria,”. amesema Ntobi

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Hamis Ngunila ameeleza kuwa  Juni Mosi mwaka huu waliandika barua kuliomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga kuutumia uwanja wa jeshi hilo Juni 7, lakini katika barua yao wakajibiwa siku hiyo Uwanja huo utakuwa na matumizi mengine.

“Tarehe 1,06,2024 tuliandika barua kwenda katika jeshi la zimamoto kwa ajili ya kuomba kutumia uwanja wa Zimamoto ambao kiuhalisia uwanja huu ni uwanja wa umma kwahiyo tuliomba uwanja ule ili tuweze kufanya mkutano wa hadhara lakini majibu yaliyotolewa ni kwamba uwanja ule Tarehe 7 ambayo ilikuwa ni siku ya Ijumaa ni kwamba uwanja ule utakuwa na matumizi mengine, tukapokea majibu hayo lakini tukafikiri kwamba kwamba kwa sababu uwanja huo siku ya Ijumaa utakuwa na matumizi tukafikiri kusogeza mbele mkutano wetu tukaandika barua nyingine kuwaomba jeshi la zimamoto kwamba badala ya siku ya Ijumaa ambayo ni tarehe 7 tufanye mkutano wetu wa hadhara wa jimbo basi tukausongeza mbele, tutaufanya wiki ijayo siku ya Jumatano tarehe 12, 06,2024 lakini cha ajabu majibu yaliyotoka ni kwamba uwanja ule wa jeshi la Zimamoto hauruhusiwi tena kufanyiwa mikutano ya kisiasa”.amesema Ngunila

“Sasa tunaujulisha umma kama kiongozi wa jimbo nikiambatana na viongozi wengine wa Mkoa kwamba ratiba ambayo tumeomba  kuutumia uwanja ule tarehe 12 wiki ijayo siku ya Jumatano iko pale pale na tumesema hivo kwa sababu kiwanja kile tumekuwa na rekodi nacho mara kwa mara tunafanyia mikutano ya hadhara lakini tambueni kuwa hatuna taarifa yoyote baada ya kuweka zuio la kufanyia mikutano ya hadhara kwenye kile kiwanja hawajawahi kutufahamisha”.

“Mambo haya yametupa mkanganyiko sana na tumeanza kuamini kuwa yawezekana ukandamizaji wa kidemokrasia kwenye taifa hili unaendelea itoshe kusema sauti hii iende kwa umma na watanzania wajue kwamba sisi kama viongozi ambao wametupa dhamana hatuwezi kukubali lazima mkutano wetu ufanyike”.amesema Ngunila

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga Martin Nyambala, amekili kuwazuia CHADEMA kufanya mkutano wao wa hadhara katika eneo hilo

“Ni kweli tulipokea barua kutoka chama cha demokrasia na maendeleo wakiomba kutumia viwanja vya zimamoto na uokoaji kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara na sisi tumewajulisha kwamba uwanja wa jeshi la zimamoto na uokoaji unamakatazo hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za kisiasa lile ni eneo la jeshi litatumika kwa ajili ya kazi za kijeshi kwa maana ya kazi za jeshi la Zimamoto na uokoaji lakini pia viwanja vitatumika kwa ajili ya kazi za kiserikali na shughuli nyingine za kijamii zisizokuwa za kisiasa ambazo zimepata kibali kutoka kwa mamlaka zinazohusika kwahiyo napenda kuwajulisha watu wa CHADEMA kwamba watafute eneo linguine ambalo wanaweza wakalitumia ambalo halina makatazo ili waweze kufanya mkutano wao ambao wanatarajia kuufanya”.amesema Nyambala

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi, akionyesha majibu ya barua za zuio la kutumia uwanja wa Zimamoto uliopo Nguzonane mjini Shinyanga.

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Hamis Ngunila akielezea hatua mbalimbali ambapo amelilalamikia jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kuwazuia kutumia uwanja huo kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara. 

Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Hamis Ngunila akielezea hatua mbalimbali ambapo amelilalamikia jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kuwazuia kutumia uwanja huo kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara. 

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga Martin Nyambala akifafanua kuhusu malalamiko ya CHADEMA Mkoa wa Shinyanga.

TAZAMA VIDEO YOTE YA CHADEMA NA MAJIBU.