Chama cha national league for democracy (nld) chajitoa uchaguzi serikali za mitaa….chamtaka jafo ajiuzulu

Chama
cha National League for Democracy (NLD) kimetangaza rasmi kujitoa
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku kikimtaka Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani
Jafo, ajiuzulu.

Uamuzi
wa chama hicho umeongeza idadi ya vyama vya siasa vya upinzani
vilivyofikia uamuzi wa kujitoa kushiriki uchaguzi huo kufikia vinane.
Vingine ni ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Chauma, NCCR-Mageuzi, UPDP, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha
Kijamii (CCK).


Kwa mujibu wa taarifa ya NLD iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa chama
hicho, Oscar Makaidi, kinamtaka Jafo kujiuzulu mara moja kwa madai kuwa
ameshindwa kusimamia uchaguzi huo na kulitia taifa hasara.
“NLD hatuna imani naye licha ya kuagiza kuwa wagombea wote
walioenguliwa, warudishwe, agizo ambalo hana mamlaka nalo kikanuni wala
kisheria,” Makaidi alisema.
Katika taarifa yake hiyo, NLD kimeamua kujitoa katika uchaguzi huo kwa
kuwa una kasoro kubwa na haziwezi kurekebishika katika muda uliobaki.
Chama hicho kimemwomba Rais John Magufuli kusitisha uchaguzi huo
unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 na mchakato wake wote uanze upya.
“Kwa kuwa Tamisemi imeshindwa kusimamia uchaguzi huu wa Serikali za
Mitaa, tunataka usimamiwe na tume huru ya taifa ya uchaguzi,” alisema.
Makaidi pia alisema NLD haikubaliani na uamuzi wa Jafo kuwa amefuta
uamuzi wote uliofanywa na wasimamizi wasaidizi kwa kuwa hana mamlaka
hayo kikanuni na kisheria.
“Tunaamini kwamba kuendelea na uchaguzi chini ya usimamizi ule ule ni
kuhalalisha upungufu wote uliojitokeza, mwingi ukiwa ni wa makusudi.
“Kuendelea na uchaguzi huu ni kuendelea kutegemea makosa mengine huko
mbeleni hasa wakati wa upigaji kura na utangazwaji wa matokeo yake.
“Tumepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagombea wetu
yanazothibitisha ukiukwaji na ubakwaji wa demokrasia kwa kiwango cha
kutisha kiasi cha kuufanya uchaguzi huu kuwa kituko.
“Kwa ujumla, uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi, hivyo
tumeazimia kujitoa,” Makaidi alieleza zaidi katika taarifa yake hiyo.
Kiongozi huyo wa NLD aliwataka wanachama na wagombea wao wote nchi nzima
kuwa watulivu na kutojihusisha kwa lolote kuhusiana na uchaguzi huo
mpaka hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.