Daktari kizimbani kwa uhujumu uchumi, kutoa mimba

Daktari
wa Hospitali ya Dental Clinic, Awadhi Juma (40) na mwenzake,
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na
kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo na ya utoaji wa mimba. Mshtakiwa mwingine
katika kesi hiyo ni muuguzi wa hospitali hiyo, Kidawa Ramadhani (26).


Washtakiwa hao kwa pamoja walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo.

Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, akisaidiana na Wakili wa Serikali
Glory Mwenda, kwa nyakati tofauti waliwasomea washtakiwa hao mashtaka
yao.

Katika
shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa Oktoba, mwaka huu, eneo la Sinza Mori,
jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa na lengo la kutoa mimba,
waliingiza bomba la sindano katika sehemu za siri za wanawake wawili
tofauti (majina yamehifadhiwa) na kusababisha kuharibika kwa mimba zao.

Ilidaiwa
kuwa Agosti, 2002 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Juma kwa lengo la
kudanganya, alighushi cheti cha Diploma cha Utaalamu wa Tiba ya Kinywa
akionyesha ni halali kimetolewa na Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi za
Afya Muhimbili wakati akijua si kweli.

Mshtakiwa
Juma pia anadaiwa kwamba Februari 20, 2015 jijini Dar es Salaam,
alighushi leseni ya biashara ya tarehe hiyo akionesha imetolewa na
Manispaa ya Kinondoni wakati akijua si kweli.

Ilidaiwa
kwamba kati ya Mei, 2015 hadi Desemba 4, mwaka huu, mshtakiwa huyo
alikutwa akimiliki hospitali ya tiba ya meno bila kibali.

Ilidaiwa
kwamba katika tarehe hizo, mshtakiwa huyo kwa nia ya kudanganya,
alijiita daktari kinyume cha sheria huku akijua si kweli.

Katika
shtaka jingine ilidaiwa kuwa katika tarehe za tukio la sita, Juma
alitakatisha na kujipatia Sh. 260,000 wakati akijua fedha hizo ni zao la
kosa la jinai la kughushi.

Upande
wa Jamhuri ulidai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi
iliahirishwa hadi Januari 10, 2020 kwa ajili ya kutajwa. Washtakiwa
walirudishwa rumande kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha hayana
dhamana.