Dc katambi aingilia mgogoro wa mirathi

 Image result for patrobas katambi
 
Na Ahmed Mahmoud,Dodoma
Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini  Patrobas Katambi ameingilia kati mgogoro wa mirathi wa watoto wa marehemu Hussein Bakari Dima wanaotaka kudhulumiwa nyumba yao na ndugu wa marehemu baba yao iliyopo eneo la Kizota Area A Dodoma mjini.
Nyumba hiyo wanayodhulumiwa watoto  hao ipo katika kiwanja namba 9 na 10 katika kitalu 34  .
Mgogoro huo  ambao ulianza takribani miezi miwili iliyopita ambapo Shangazi na baba mdogo wao walikuja na hoja ya kutaka kuwakabidhi mali za urithi wa marehemu baba yao kwa kuwa watoto hao wamekwisha kuwa wakubwa na umri Zaidi ya miaka 18 na wanaweza kujitegemea.
Wakielezea sakata hilo  watoto hao Omar Hussein (29) na Shamila Hussein (26)walitaka kufahamu mali ambazo shangazi yao anataka kuwakabidhi,lakini kinyume na matarajio yao shangazi yao alikuja na watoto wengine wawili akidai ni watoto wa nje ya ndoa wa marehemu ambao wanastahili kugaiwa nyumba hiyo ambayo tangu marehemu baba yao akiwa hai alishawarithisha.
“Sisi tulikataa ombi la shangazi ndipo alipoamua kwenda mahakamani kufungua ombi la kutaka kuwa msimamizi wa mirathi bila kutushirikisha wala kuwa na kikao cha familia ambacho kimemteua na kuwa na muhtasari wa kumkubalia kuwa msimamizi wa mirathi”.alisema Omar.
Omar alisema baada ya shangazi kufungua kesi hiyo iliyosikilizwa kwa siku mbili na kutolewa hukumu licha ya kuwa hawajui sheria lakini hawakuridhishwa na uamuzi huo uliompa shangazi yao haki zote za kuwa msimamizi wa mirathi ikiwemo  kuiuza nyumba yao na kumgaia mtoto anaeona anafaa au angependa.
“licha ya kumuomba Rais wetu Magufuli atusaidie tusidhulumiwe haki yetu tuliamua kwenda kwa mkuu wa wilaya kupeleka malalamiko yetu tukijua kuwa ndipo tunaweza kupata haki,kwa kuwa hatuna uwezo wa kifedha na mahakamani hatujasikilizwa licha ya kuwa na hati halali za umiliki wa nyumba yetu, lakini Hakimu alisema ni za kughushi bila kututhibitishia, shangazi ambae hakuwa na nyaraka yeyote alisikilizwa na kupewa haki ya kuwa msimamizi wa mirathi”alisema Omary.
Baada ya kupokea malalamiko ya watoto wa marehemu yaliyofikishwa kwa Mkuu wa wilaya ya Dodoma  yakionesha kutoridhishwa na uamuzi wa mahakama ya mwanzo ya Makole iliyotolewa Oktoba 28 na Hakimu Nduka iliyompa mamlaka shangazi yao  Zakhia Said kuwa msimamizi wa mirathi bila wao kusikilizwa watoto hao.
Omary alisema nyumba hiyo ilijengwa na baba na mama yao wakati wa uhai wao,ambapo baba yao alifariki mwaka 1998 na mama yao alifariki mwaka 2010, ambapo wamesisitiza kuwa tangu baba afariki hii nyumba ilikuwa chini ya umiliki wao wakisimamiwa na marehemu mama kwa kuwa walikuwa bado wadogo ambapo wamemshangaa shangazi kuja na hoja ya kutaka kugawa mali za marehemu baada ya miaka 21.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa wilaya ya Dodoma baada ya kufikishiwa malalamiko hayo na kuyapitia alitumia uamuzi wa kumuita shangazi yao afike katika ofisi yao ili kujua undani wa suala hilo ambapo alidai kuwa yupo mkoani Kilimanjaro.
Katambi amesema  kuwa, namna alivyolitazama suala hilo alibaini kuwepo dosari nyingi za kisheria baada ya kuangalia mlolongo wote ameona kumekuwepo na  ujanja ujanja  baada ya kuangalia nyaraka zote.
“Hatua ya kwanza nimeona niongee na hakimu mfawidhi ili aweze kuangalia mwenendo mzima wa shauri hilo jinsi ambavyo limeenda”alisema Katambi.
Aliongeza kuwa, wao kama serikali hawana wajibu wala haki ya kuingilia mahakama ila tuna haki ya kusimamia utaratibu,sheria kwa maana utawala wa sheria pale wanapoona kwamba kuna viashiria vya kupindishwa kwa sheria au kutokuwepo kwa misingi mizuri ya usimamizi wa sheria na haki hapo ndipo wanaingia kama sehemu ya serikali.
“nimefika hapa ili kwanza nilielewe eneo lakini pia kupata nyaraka hizo na pili kuwapata hao wanaolalamikiwa ili tuweze kupima na kuangalia haki iko wapi kwa hiyo tutafanya vizuri kabisa kwa kushirikiana na mahakama kuweza kuona haki ya watoto hawa inapatikana na hawadhulumiwi.”alisema Katambi