Dc simanjiro ahamia kwenye lango la ukuta wa magufuli




*************************************

MKUU wa Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula ameagiza vituo vya
kuandikisha wapiga kura katika vituo vya vitongoji 24 vya Mji mdogo wa
Mirerani kuhamia kwa muda kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta
unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ili kuwapa watu wengi fursa ya
kujiandikisha. 
 

Mhandisi Chaula
alisema shughuli ya uandijishaji imehamishiwa kwa muda kwenye eneo hilo
ila vituo husika vitaendelea na kazi hiyo baada ya kukamilika kwa
uandijishaji katika lango hilo. 
 

Alisema tangu asubuhi
ya leo wamefanikisha kuandikisha watu 2,111 kupitia vitongoji 24 vya
kata mbili za Mirerani na Endiamtu katika mji mdogo wa Mirerani.
 

“Baada ya kuona
shughuli ya uandikishaji inasuasua kwenye mji mdogo wa Mirerani na
Orkesumet kamati ya usalama ikaamua kuweka mikakati ya kufanikisha
uandikishaji,” alisema mhandisi Chaula. 
 

Alisema hadi hivi
sasa watu 81,400 wamejiandikisha wilayani humo kati ya makisio ya
wananchi 105,052 wanaotarajiwa kujiandikisha sawa na asilimia 85.
 

Alisema anatarajia wananchi wengi watajiandikisha na hadi sasa wanatarajia kufikia asilimia 90 na leo watamalizia zilizobakia. 
 

“Nawashukuru wananchi
wote kwa kujitokeza kujiandikisha na wasimamizi wa uandikishaji huo
kwani agizo la Rais John Magufuli la kutaka wenye sifa washiriki
uchaguzi huo linafanikishwa,” alisema mhandisi Chaula. 
 

Hata hivyo, ameagiza
vitongoji na vijiji vya wilaya hiyo kufanya mikutano yao siku ya mwisho
ya kujiandikisha ili wakamilishe kwa kila mmoja kutumia haki yake ya
kujiandikisha. 
 

Mmoja kati ya
waliojiandikisha kwenye lango hilo Mohamed Hassan alisema yeye ni mkazi
wa Kitongoji cha Zaire na ameshajiandikisha kabla hajaingia ndani ya
lango hilo. 
 

“Kuna baadhi ya watu
wanaopanda kwenye migodi ya Tanzanite wamepata fursa ya kujiandikisha
baada ya mkuu wa wilaya kuagiza shughuli hiyo ifanyike hapa kwa muda,”
alisema Hassan.