DED Kasulu atekeleza agizo la Mpango,

Na Respice Swetu, Kasulu

Baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philip Isidor Mpango kupita katika kijiji cha Nyakitonto alipokuwa ziarani mkoani Kigoma na kutoa agizo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kufanya mkutano na wananchi wa kijiji hicho, agizo hilo limetekelezwa.

Siku moja baada ya agizo hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dr. Semistatus Mashimba akifuatana na baadhi ya wataalamu kutoka katika ofisi yake, amezungumza na wakazi wa kijiji cha Nyakitonto kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu, Dkt Mashimba aliyevaa miwani aliyekaa katika meza mbele akisikiliza hoja za wananchi (hawaonekani pichani) katika Kijiji Cha Nyakitonto ikiwa ni agizo la Makami wa Rais Dkt. Philip Mpango alilolitoa hivi Karibuni.

Katika mkutano huo wakazi wa kata ya Nyakitonto wakiongozwa na diwani wa kata hiyo Daniel Nzababa, pamoja na kupata fursa ya kukutana na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, waliutumia mkutano huo kuwasilisha hoja mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na zilizohusu ardhi, huduma za afya, huduma za maji, huduma za elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, miundombinu na ushirikishwaji.

Akijibu hoja hizo Dr. Mashimba ambaye amehamia katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu hivi karibuni kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino iliyopo mkoani Dodoma amesema, nia yake ni kuona wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu wakifanya shughuli zao bila usumbufu kutoka kwa watu wanaokiuka maagizo ya serikali.

Amesema lengo lake ni kuiona Nyakitonto na halmashauri nzima ya wilaya ya Kasulu inapata maendeleo ambapo hatua mbalimbali zinapaswa kuchukuliwa na kuwatahadhalisha wananchi wa Nyakitonto na wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kuwa mchakato wa kuyafikia maendeleo hayo una gharama.

Dr. Mashimba amezitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na kutenga maeneo yatakayotumika kwa ajili ya kujenga viwanda na taasisi kama mabenki, TRA, maduka, sehemu ya kuegesha malori, kituo cha biashara, na vituo vya mafuta.

“Eneo hili lipo kwenye makao makuu ya halmashauri halitakiwi kuendelea kuwa hivi, linatakiwa kupimwa na kupangwa vizuri, jiandaeni kwa mabadiliko na kuwa tayari kutoa sehemu ya ardhi kwa ajili ya upitishaji wa miundombinu ya barabara, maji na kuchangia gharama za urasimishaji na kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi”, amesema.

Pamoja na mkutano huo kufanyika kutokana na agizo ya Makamu wa Rais, tangu kufika kwake Dr. Mashimba amefanya ziara kwenye vijiji na kata na mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa lengo la kufahamiana, kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.