Diamond akabidhi kwa serikali hoteli yake itumike kama hospitali ya kuhudumia wagonjwa wa corona au kama karantini

Staa
wa muziki nchini Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz  ametoa
ruhusa kwa serikali kuitumia hoteli yake mpya aliyoinunua kama hospitali
ya kuhudumia wagonjwa wa corona au kama karantini.


Diamond
amesema hayo leo ikiwa ni siku mbili baada kutangaza kuwalipia nyumba
watu 500 ili kuondokana na adha ya kodi katika kipindi hiki cha
maambukizi ya ugonjwa wa covid-19.

“Misukumo
ya kusaidia watu, imetokana na malezi niliyolelewa, maisha niliyotokea
na historia yangu ya nyuma. Nikikumbuka shida nilizopitia, napata moyo
wa kusaidia wengine.

“Nimenunua
hotel maeneo ya Mikocheni B, jijini Dar es Salaam ina vyumba zaidi ya
30, nimeshakabidhiwa documents zangu, ipo kwenye marekebisho kadhaa
kisha nitaitambulisha. Kwa sababu sijaanza kui-upgrade, niko radhi
niitoe kwa serikali kwa muda huu ili iweze kutumika kama Karantini au
Hospital mpaka pale Corona itakapoisha,” amesema Diamond.

Aidha,
Mondi amesema hajaweka kiwango cha mwisho cha kodi atakazowalipia
wananchi, lakini lazima ataangalia wenye uhitaji haswa. Kwa sababu wapo
wanaolipa pesa kubwa mpaka Tsh million 1 kwa mwezi, na mwengine Tsh
60,000 tu na inawashinda.

“Sitaangalia
Dar es Salaam peke yake, ntajitahidi na kila mkoa nisaidie walau
familia tano. Kwa sababu mikoani pia kuna watu wana shida sana.
Sitaangalia jinsia moja zaidi, nitaweka usawa kwa wote. Kwa sababu suala
la kodi linamgusa kila mtu, wanawake kwa wanaume.

“Ili
kuweza kuwafikia walengwa halisi wanaotakiwa kufaidika na hizi kodi,
tutatumia serikali za mitaa. Watu wapo wengi lakini lengo ni kuwafikia
masikini, wajane, na wale wasio na uwezo. Baada ya hili la kodi kuisha,
nitakuja na mpango wa kuwasaidia Ma-DJ wa ma-club na redio. Kwa sababu
ni miongoni mwa kundi lilioathirika sana na kipindi hiki cha Corona,”
amesema.