Dkt. gwajima aweka reheni vyeo vya watumishi makore dodoma



Wananchi walikutwa katika kituo cha Afya makore wakipata huduma siku ya tareh 02,Novemba, 2019


Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Dkt. Dorthy Gwajima, akizungumza katika zoezi la ufatiliaji kwenye kituo cha Afya Makore.


Mmoja wa Wafamsia katika kituo cha Afya Makore, akisajili dawa kwenye kitabu cha kupokelea Ledger.


 Watumishi wa Kituo cha Afya Makore wakiwa wanapewa somo wakati wa Ziara hiyo na Naibu Katibu Mkuu.


 Eneo la Stoo yakutunzia dawa katika kituo cha Afya Makore.


Mtekinolojia Maabara kama alivyokutwa wakati wa Ziara ya Naibu Katibu Mkuu.



Godfrey Mahundi Msimamizi wa
Maabara katika kituo cha Afya Makore akitoa maelezo mbele ya naibu
katibu Mkuu wakati wa ziara hiyo ya kikazi. 



Na. Atley Kuni- OR-TAMISEMI


Baadhi ya
watumishi wa Afya katika Kituo cha Afya Makore mkoani Dodoma wamejikuta
kwenye wakati mgumu mara baada ya kubainika kufanya kazi kinyume na
taratibu zinavyo elekeza. Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Daktari Dorothy
Gwajima amesema, kutokana na kukithiri kwa utendaji wa mazoea kwa
baadhi ya watumishi wanaopima upepo sasa kaguzi zote zitaanza kufanyika
kwa mwelekeo wa kutathmini jinsi gani kila mtumishi wa kada husika
ametekeleza majukumu yake kama yalivyoelekezwa kwenye muundo wake wa
utumishi.


Aidha, amewaeleza
watumishi hao kuwa, inaonekana maboresho yanayoonekana katika kituo
hicho yakawa yanafanywa na watumishi wachache wanaofidia utegaji wa
wengi hivyo, kutokana na mwenendo huo sasa hatasita kuwashtaki wazembe
wote kwa Katibu Mkuu utumishi ili hii habari ya kupandishana vyeo iende
sambamba na chujio makini la ufanisi wa kila mtumishi na kiongozi mahala
pa kazi.


Hatua hiyo
imekuja kufuatia ufuatiliaji endelevu unaofanywa na Naibu Katibu Mkuu na
jopo la wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kituo hicho na
vingine nchini ambapo, kituo cha afya Makore ni mojawapo ya vituo
vinavyojengewa uwezo viwe vya mfano katika mabadiliko ya mifumo ya
uwajibikaji mahala pa kazi. Mwelekeo huu ni utekelezaji wa mojawapoa ya
Azimio la Kikao cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika
Agosti, 2019 kuwa, kila halmashauri iteue vituo 4 vya mfano.


 “Sitasita
kumshauri Katibu Mkuu Utumishi asiridhie baadhi ya watumishi miongoni
mwa 80 mnaowaombea wapandishwe vyeo iwapo nitabaini ufanisi wao hautoshi
kupitia kaguzi tunazofanya. Nitamwambia Katibu Mkuu hawa
watumishi hawastahili kupanda vyeo kwakuwa wameshindwa kutekeleza wajibu
wao ipasavyo na hapa msisingizie eti mko wachache wakati idadi yenu ni
mara mbili ya wanaotakiwa hapa,” alisema Gwajima na kusisitiza
kuwa,“haiwezekani zaidi ya miezi mitatu wataalamu wa kitengo cha dawa
eti hawajahuisha taarifa za dawa kwenye kitabu husika (Ledger) yaani
mnajifanyia fanyia tuu bila utaratibu halafu mnasema dawa hazitoshi huku
mmeotesha vichaka vyenye utata wa kujua wapi mmezitumia?” alihoji
Gwajima.


Katika ziara hiyo
Naibu Katibu Mkuu pia, alifanya uhakiki wa hadi ujazo wa kila
kitendanishi cha maabara kwamba kilitakiwa kupima sampuli ngapi na
mwisho kimepima ngapi ambapo, alibaini wataalamu wa maabara wamepima
sampuli nyingi zaidi kuliko walizotakiwa kupima huku wakiwa hawana
kumbukumbu za kiofisi kuhusu wapi walikopata vitendanishi vya ziada,
‘inakuwaje ulitakiwa kwa kitendanishi hiki upime sampuli 50 badala yake
umepima 350”? Gwajima alihoji.


Naye mtaalamu wa
Maabara katika kituo hicho Ndugu Godfrey Mahundi hakuwa na majibu yakina
juu ya wapi hasa alitoa ziada hiyo ya vitendanishi na kama ipo sehemu
alikotoa kwa nini hakuna rekodi ya aliyempa wala yeye kukiri mapokezi.


Dkt. Gwajima
alisema, kwa kawaida taratibu za uchukuaji dawa lazima ziwe 
zinaandikishwa kutoka eneo moja hadi lingine yaani kutoka hifadhi kuu,
hifadhi ya kati, hifadhi ndogo mpaka zinapomfikia mgonjwa na hata kama
amepewa toka kwenye kituo kingine lazima kuwe na rekodi za aliyetoa na
aliyepokea.


“Hapa Kituo cha
Afya Makore baadhi ya watumishi wameelewa somo hasa eneo la huduma za
kitabibu na kiuguzi ila nyie watu wa maabara na dawa ndiyo bado mnapima
upepo mnajifanyia mambo kienyeji kwa kutoandika kumbukumbu za matumizi
ya raslimali za dawa na vitendanishi na nani katumia, nasema nyie pamoja
na wengine wote nchi nzima wanaofanya mambo kama yenu ambayo,
yanayoruhusu kushamiri kwa vichaka vya matumizi mabaya ya raslimali za
vituo sasa wakati umefika wa kuamua kurudi kwenye mstari ama mtausikia
tu utumishi wa umma kwenye redio. Aliendelea kusisitiza Katibu Mkuu.


Amesema kituo
hicho ni cha mfano na watakaofanya hapa lazima wawe wa mfano na si
vinginevyo, huwezi kuwa mtumishi wa kituo cha mfano huku wakitoa fursa
ya majizi kujificha kwenye kazi zao. Ameongeza kuwa ijulikane kuwa hizo
 ni salamu zake kwa vituo vyote vya afya nchini.


Katika hatua
nyingine Watumishi hao walionesha kutambua uzembe walioufanya na kukiri
kuzembea katika utendaji wao huku wakiomba msamaha na kuahidi
kubadilika.


Akikiri kufanya
uzembe Mfamasia wa Jiji la Dodoma George Hondi, kwa niaba ya watumishi
wengine, alisema wanaona fedheha na aibu kwani yote yaliyobainishwa na
Naibu Katibu Mkuu hakuna hata moja la kusingiziwa wala kuonewa.


“Ni kweli hatujatekeleza na kusimamia majukumu yetu na hili ni kosa na sisi tuseme tu na kunaahidi kubadilika” alisema Hondi.


Kwa mujibu wa
Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Namba 1 wa Mwaka 2009 unaoeleza juu ya
Miundo ya Utumishi kwa Kada za Afya chini ya Wizara ya Afya yapo mambo
mengi ambayo yameendelea kugundulika kupitia ziara hii na zingine za
Naibu Katibu Mkuu na timu yake na yanayotokana na baadhi ya watumishi
kujifanyia kazi kienyeji mfano, Mfamasia Daraja la Pili anayo majukumu
yake ikiwemo kutunza kumbukumbu za dawa na vifaa tiba na kutekeleza
maelekezo ya wizara kuhusu ufanisi wa Kamati ya Dawa kwenye kituo husika
lakini wengi hawafanyi na sababu hawana lakini wanadai wapandishwe vyeo
Hii haiwezekani” amesema Dkt Gwajima.  


Chini ya
OR-TAMISEMI imeundwa timu rasmi ya kuwa inafanya ukaguzi wa utekelezaji
wa majukumu ya kila mmoja tutajua huko huko wapi hawatoshi na wapi wako
idadi kubwa lakini hawana tija.


Dkt. Gwajima
amewataka Makatibu wa Afya kutokuwa makarani wa kuorodhesha tu majina ya
watu kupanda vyeo kisa mtumishi kaajiriwa siku nyingi bali wapime
ufanisi ili kumtendea haki anayejituma na mzembe naye apate haki yake ya
kutopandishwa cheo au kushushwa. Amesema wataimarisha mifumo na
taratibu za kujipima na kuwapima watumishi ili haki itendeke haraka kwa
wale wanaojituma na wasiojituma pia wapate haki yao mapema tu kila mtu
abebe mzigo wake.


Mapema juma
lililopita, Naibu Katibu Mkuu akifungua Kikao cha Wafamasia wa Mikoa
mjini Dodoma, aliwarushia lawama wataalam wa Afya hususani kada ya
Famasia kwamba, wizi wa dawa unaoshamiri unachangiwa na usimamizi mbovu
eneo lao kiasi kwamba dawa hizo zinapotea bila taarifa kwa kuwa
hawazingatii au kwa makusudi wanafanya kazi huku wakitoa fursa nzuri kwa
wezi na wadokozi kutekeleza azma yao na hii ni kusaliti juhudi za
Serikali za kuongeza bajeti ya dawa na kufikia bilioni 269, hivyo akaapa
kupambana nao kwa kuomba nguvu za wananchi kuwafichua wote
watakaobainika kuhujumu jitihada hizo.


Ofisi ya Rais
TAMISEMI, kwa mujibu Muongozo wa sasa ndio msimamizi Mkuu wa Hospitali
za Wilaya, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati kote nchini.