Dkt. mollel: taulo za kike zisambazwe kama kondom

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akizungumza katika banda la Okoa New Generation katika Maadhimisho ya Hedhi Salama Jijini Arusha.

Egidia Vedasto 

Arusha 

Wadau wa hedhi salama wametakiwa kuhakikisha taulo za kike zinakuwepo katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama inavyosambazwa kondom.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Arusha Naibu Waziri  wa Afya Dkt.Godwin Mollel amesema serikali, wadau na jamii kwa ujumla ni muhimu kuchukulia  uzito suala la hedhi Salama kwani Hedhi Salama ni Uhai.

“Nawakumbusha wazazi kwamba msichukulie kwa usawa katika mahitaji ya watoto kwani watoto wa kike wana mahitaji ya ziada ya kila mwezi ili waweze kujisitiri na kufurahi wakati wote” amesema na kuongeza.

“Ni vyema maeneo yenye mikusanyiko kama sokoni, shuleni, hospitalini na hotelini zikawepo na sisi serikali tunaendelea kufanya jitihada za kuongeza vyumba vya kujisitiri katika maeneo hayo ili kutimiza adhma ya mazingira rafiki ya hedhi salama” amesema Dkt. Mollel.

Hata hivyo Dkt. Mollel ameeleza kwamba asilimia 75% ya watumiaji wa taulo za kike ambao ni wanafunzi wamependekeza taulo za kufua ambazo hudumu kwa muda mrefu, na kuahidi Serikali kukaa na Wizara ya Fedha kuangalia namna ya kupunguza kodi kwa wadau wanaozalisha na kusambaza  taulo hizo shuleni hasa maeneo ya vijjijini.

Kwa upande wake mmoja wa wadau wa Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania, na  Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia isiyokuwa ya Kiserikali ya TASACI inayojihusisha na kuwajengea wananchi  uchumi kupitia vikundi, kufundisha nidhamu ya fedha, ujasiliamali, afya bora na kijinsia, upandaji miti na utunzaji wa mazingira, uwajibikaji na utawala bora Japheth Mswaki, amesema hedhi salama inahusisha jamii nzima ambao ni Mama, baba, watoto na wadau wengine katika jamii.

Mmoja wa Wadau wa Jukwaa la Hedhi SalamaTanzania na Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia isiyokuwa ya Kiserikali ya (TASACI) Japheth Mswaki.

Amesema sambamba na majukumu mengine ya asasi hiyo wanajikita katika kuhakikisha jamii inatambua umhimu wa hedhi salama ambao si kwa akina mama pekee bali baba ni muhimu hivyo ni vyema atambue nafasi yake katika mchango wa hedhi salama.

“Huduma hii inahitaji kujitoa katika uchangiaji ili kuhakikisha upatikanaji wa taulo za kike shuleni, sokoni na sehemu nyingine katika jamii, na suala hili linaenda sambamba na lishe bora, makuzi bora, tabia, malezi na mahitaji” ameeleza Mswaki.

Mkurugenzi wa Shirika la Okoa New Genegeration lilopo Jijini Arusha  wanaozalisha taulo za kike za kufua Neema Mgendi amesema wanajikita katika kusaidia wasichana wenye ulemavu, wasichana wa kazi za ndani na wanawake wengine walio katika mazingira magumu ambao mara nyingi hawafikiwi na  huduma hizo.

“Unaweza kuona kwa mfano hapa katika maadhimisho hakuna msichana wala mama mwenye ulemavu, hivyo ni jukumu letu kuwaibua na kuwafikia popote walipo na kuwapa huduma za taulo na sabuni ili kuwaweka salama katika kipindi cha hedhi” amesema Mgendi.

Grace Mashele kutoka kiwanda cha  AtoZ cha Jijini Arusha amesema taulo hizo zinadumu kwa miaka miwili baada ya mifuo mia moja ambapo dawa ya kuzuia fangasi na bakteria huendelea kupungua.

Grace Mashele kutoka kiwanda cha AtoZ akiwa katika banda la maonyesho ya hedhi salama.

“Kiwanda chetu tunazingatia makundi mbalimbali katika jamii na bei ni elekezi kuhakikisha watoto wa kike hasa walioko shuleni wanapata huduma hiyo katika kipindi cha hedhi” amesema Mashele.