Ebola : who yaikosoa tanzania kwa kutotoa ushirikiano

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeikosoa Serikali kwa kutotoa
ushirikiano juu ya taarifa za uwezekano wa kuwepo matukio ya Ebola
nchini humo.
 

Shirika limeeleza katika taarifa yake kuwa lilipata taarifa kuna
mgonjwa mmoja aliyeshukiwa kuwa na maambukizo hayo aliyefariki Dar es
Salaam, na wagonjwa wengine wawili lakini hata baada ya shirika hilo
kuomba mara kadhaa taarifa juu ya matukio hayo, halikupewa ushirikiano.

Hata hivyo Tanzania imesema kuwa haina mgonjwa yoyote anayeshukiwa kuwa na Ebola au kuthibitishwa kuwa na virusi.

Katika mlipuko wa hivi karibuni Ebola imeuwa zaidi ya watu 2,000 huko
mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati Uganda
ikiendelea kupambana kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Ugonjwa huo wenye kuambukiza kwa kasi uliathiri baadhi ya maeneo ya
Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016 na kuua zaidi ya watu
11,000.

Nini ambacho WHO inakilalamikia?

Tamko lake la Jumapili limesema kuwa Septemba 10, 2019, shirika hilo
lilipata taarifa kuwepo kwa mgonjwa anayeshukiwa kuwa na maambukizo
mjini Dar es Salaam, mji uliokuwa na watu wengi zaidi Tanzania, katika
kile ambacho kinasadikiwa kuwa ni tukio la kwanza la Ebola nchini.

Tamko hilo lilieleza kuwa mgonjwa huyo alikuwa nchini Uganda,
akaonekana na dalili za Ebola Agosti, 2019, akapimwa na kuonekana na
virusi, alifariki Septemba 8, 2019. Watu waliokutana na mwanamke huyo
waliwekewa karantini.

WHO inasema ina taarifa ambazo sio rasmi za uwezekano wa kuwepo wagonjwa wengine wawili.