Gambo tena, kikongwe amshushia tuhuma nzito, dc jerry muro na yeye atupiwa lawama na kikongwe arumeru

Na Ahmed Mahmoud Arusha

WAZIRI wa Ardhi nyumba na makazi ameombwa kuingilia kati mgogoro wa
ardhi uliodumu kwa miaka kumi kati ya Bi Angaza Selemani (85) na Elias Barnabas Chami pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Mashaka Mrisho Gambo.

Katika barua yenye kumbukumbu namba 01/M/D/RC/AR/2019 ya Novemba 23
2019 iliyoandikwa na Bi Angaza kwenda kwa William Lukuvi anamlalamikia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa manyanyaso anayoyapata.

Barua hiyo ambayo blog hii imefanikiwa kuona nakala yake Kikongwe
huyo anamlalamikia Gambo kwa kushindwa kumsaidia katika mgogoro wake
na mtoto wa aliyekuwa mpenzi wake.

Katika barua hiyo Bi Angaza anamtuhumu Gambo kwa kudai amechukua fedha zake kiasi cha  Tsh 2,000,000 zilizokuwa katika akaunti yake katika Benki ya biashara ya NBC kwa kuwa salio lililokuwa katika akaunti hiyo limeyeyuka pasipo yeye kujua zilipoenda.


“Nilipofika benki kutaka kutoa fedha zangu nilikuwa hakuna kitu lakini nimeingiwa na hofu inawezekana fedha hizi zimechukuliwa na Gambo kwa kuwa yeye ndio niliempatia namba zangu za akaunti kwa biashara ya kiwanja ambayo alitaka kuifanya na mimi,”ameandika katika barua yake hiyo.

Amedai kuwa jambo hilo linampa mashaka kuwa kulikuwa na kutengeneza mazingira ya kutaka kumtapeli shamba lake lenye ukubwa mita za mraba 63 kwa 33 katika eneo lililoko Kata ya Kimandolu mtaa wa kijenge juu halmashauri ya jiji la Arusha.

Bi Angaza amedai katika barua hiyo kuwa chanzo cha mgogoro huo ni yeye baada ya kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuomba msaada wa kutatuliwa mgogoro kati yake na  Elias Barnabas Chami ambaye alimnyang’anya sehemu ya shamba na nyumba.

Katika barua hiyo Bi Angasa anadai kuwa Gambo badala ya kumsadia kumaliza mgogoro huo alimshawishi amuuzie shamba hilo kwa milioni 70 ili amuondolee mgogoro huo na kumtaka ampatie akunti namba ya Benki .

Bi Angaza anadai katika barua hiyo kuwa baada ya kutekeleza agizo
hilo,alielezwa na Gambo kuwa aende Benki ya NBC kusaini hati ya
kupokea milioni 70, na baada ya kufika Benki alielezwa na maafisa wa  Benki hiyo  asaini hati ya kupokea pesa hizo jambo ambalo alilikataa hadi apewe pesa zake zote mkononi.

Anaendelea kudai kuwa baada ya kukataa maofisa wa Benki walimtaka
aondoke,na kumlazimu kurudi kwa Mkuu wa Mkoa Gambo ili amueleze
alichojibiwa na maofisa wa Benki na alipofika kwa Mkuu wa Mkoa aliambiwa kuwa amekataa kusaini ile karatasi basi hawezi kumsadia tena.

Katika barua hiyo anamuomba Waziri William Lukuvi amsaidie kumrejeshea shamba lake na nyumba huku akisisitiza kuwa yeye  hana mtoto wala mtu wa kumsaidia kwa sasa.

Anaeleza kuwa baada ya changamoto hiyo alimfuata mkuu wa wilaya ya
Arusha Gabriel Daqarro ofisini kwake lakini kutokana na miguu kuuma
alishindwa kupanda juu na hata hivyo mkuu huyo wa wilaya pia alishindwa kumfuata kumsikiliza licha ya kupewa taarifa za uwepo wake.

Alidai kutokuwa na imani na uongozi wa mkoa licha ya
kuingia mkuu wa mkoa mpya Idd Kimanta huku akiweka tumaini lake kwa
waziri Lukuvi kuweza kumsaidia kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Juhudi mbali mbali za kumtafuta aliyekuwa mkuu wa
mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kuzungumzia suala la kikongwe huyu zimegonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana na hata ujumbe mfupi aliotumiwa kutoujibu.

Aidha jitihada za kumtafuta meneja wa benki ya NBC Tawi la Boma Road ili aweze kujibu tuhuma hizo zilizoelekezwa kwa benki hiyo pia hazikufanikiwa kwa kuwa simu yake iliita kwa siku nzima ya bila majibu na alipofuatwa ofisini wasaidize wake walidai ametoka nje ya ofisi kikazi.


Katika hatua Nyingine

Kikongwe mwenye umri wa Miaka 94,Ndesinio Ndewario Nko Mkazi wa Kijiji cha  Nkoaranga,Wilayani Arumeru ,Mkoani Arusha,amemwomba Rais John Magufuli kumsaidia kupata eneo lake baada ya kushinda kesi mahakamani lakini uongozi wa wilaya umeshindwa kutekeleza amri ya Mahakama.

Akiongea kwa uchungu na vyombo vya habari ,Ndesinio alisema kuwa alishitakiana na mtoto wake aitwaye Emmanuel Nko ambaye aliuza kinyemela eneo hilo lenye ukubwa wa ekari moja lililopo eneo la Kiwawa wilayani humo.

Alisema katika kesi mbalimbali zilizounguruma kuanzia baraza la Ardhi la Kata,baraza la wilaya, Mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa alishinda na Mahakama hizo kumtambua yeye kama mmiliki halali wa eneo husika.

Kikongwe huyo alieleza kuwa  kijana wake huyo  aliuza eneo hilo kinyemela  mwaka 2012 kwa Ester Palangyo (Mama chai Jana) mkazi wa Maji ya chai wilayani humo bila kuishirikisha familia wakati akijua si Mali yake nani kinyume cha sheria.

Baada ya kumalizika kwa kesi hiyo ,Mahakama ya rufaa ilitoa maelekezo kesi hiyo irejeshwe baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ambao walitekeleza amri ya mahakama ya rufani kwa kukabidhi eneo kwa mdai.

Baraza hilo la Ardhi na Nyumba la wilaya la Arusha lilimwandikia barua Mkuu wa wilaya ya Arumeru yenye kumbukumbu namba DLHT/MISC.APP.NO.48 ya mwaka 2013 kuitambulisha kampuni ya udalali ya REGIZ COMPANY LTD kwa ajili ya utekelezaji wa Amri ya baraza katika shauri namba 48/2013 ya mdai Ndesinio Ndewario dhidi ya mdaiwa  Immanuel Ndewario Nko.

Alisema kuwa Kampuni ya udalali ya Regiz kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba RGZ/AR/48/2020 ilitekeleza hukumu ya shauri hilo namba 48/2013 ikiwa ni pamoja na kuondoa nyumba zilizokuwa zimejengwa na kumkabidhi mdai mbele ya watendaji wa ofisi ya kata ya Imbaseni.

Bibi huyo alidai kwamba julai 23,2020 alipokea barua kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Arumeru,Jerry Muro yenye kumbukumbu namba DC/ARUM/W.10/1XL/62 ya kusitisha kufika katika eneo hilo jambo ambalo amedai ni ukiukwaji wa amri ya Mahakama na kumtaka rais John Magufuli kuingilia kati na msaidia kupata eneo lake kwani ofisi ya Mkuu wa
wilaya inajinufaisha kupitia mgogoro huo uliokuwa umemalizwa na Mahakama.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jerry Muro akiongelea suala hilo ofisini kwake alisema kuwa ni kweli ofisi yake imesitisha utekelezaji wa Amri hiyo ya mahakama baada ya kuwepo kwa viashiria ya uvunjifu wa amani.

Akiongelea suala hilo alisema kuwa hawezi kutekeleza amri ya sasa inayotoka baraza la Ardhi wakati kuna amri nyingine ya nyuma ya Mahakama kuu juu ya shauri hilo ambayo ulitolewa na ilikuwa haijatekelezwa.

“Hapa lazima muelewe kwamba kuna amri mbili zilizotolewa na mimi naanza kutekeleza amri ya Mahakama ndio maana nimesitisha kwanza amri ya sasa ya baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya “alisema Murro

Kabla ya kusitisha kwa Amri hiyo Mkuu huyo wa wilaya aliwahi kusaini hati ya utekelezaji wa Amri ya Baraza Kupitia barua ya kampuni ya udalali ya REGIZ yenye kumbukumbu namba RGZ/MB/AR/48/2020 iliyosainiwa Mei 19 ,Mwaka huu 2020.



Kikongwe Ndesinio Ndewario