Halmashauri uvinza yamkera naibu waziri mabula

Na Munir Shemweta, WANMM UVINZA

Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
ameijia juu halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma kwa kushindwa
kuihudumia idara ya ardhi na kusababisha watumishi wa idara hiyo
kugharamia baadhi ya vifaa ili kutekeleza majukumu yao.


Hali
hiyo ilibainika jana katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwa katika ziara yake ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa kigoma.

Akiwa
katika Masijala ya Ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Uvinza, Dkt Mabula
alibaini utunzaji majalada ya ardhi usiofuata taratibu huku baadhi ya
hati zikiwa hazijakamilishwa kwa ajili ya kuwapatia wamiliki wa ardhi
katika halmashauri hiyo tangu mwaka 2018.

Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwajia juu watumishi wa
sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo kwa kushindwa kutekeleza
majukumu ipasavyo jambo alilolieleza kuwa linachangia uwepo migogoro ya
ardhi sambamba na kuwanyima wananchi fursa ya kupata hati.

Dkt
Mabula aliagiza hati zote ambazo taratibu zake zishakamilishwa ikiwemo
wamiliki wake kusaini hati hizo kupelekwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa
Ardhi Kanda ya Magharibi ndani ya wiki moja  kwa ajili ya kukamilishwa
na kupatiwa waombaji.

Hata
hivyo, baada ya kuwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika
halmashauri ya Uvinza ndipo Afisa Ardhi wa halmashauri hiyo Manyama
Makongo alipomueleza kuwa idara hiyo inashindwa kutekeleza majukumu yake
kutokana na kukosa vifaa jambo lililosababisha kuamua kuchukua 
‘Printer’ yake binafsi na kuipeleka kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya
kusaidia kazi za idara.

Hali
hiyo siyo tu ilimshutua na kumshangaza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi bali ilimsononesha kwa kuona watumishi wa sekta ya
ardhi katika halmashauri hiyo wanatumia fedha zao za mifukoni kuendesha
ofisi jambo alilolieleza kuwa halikubaliki.

‘’Hapa
jitihada za ziada zinahitajika, halmashauri ipo inashindwa kuihudumia
idara ya ardhi, halafu watumishi wanatumia fedha zao za mfukoni hili
halikubaliki lazima niwasiliane na Waziri Jafo kuhusiana na suala hili’’
alisema Dkt Mabula.

Kwa
mujibu wa Naibu Waziri Mabula, idara za ardhi katika halmashauri nyingi
nchini zimekuwa kama watoto wa kambo kutokana na wakurugenzi wa
halmashauri kutozitengea bajeti ya kutosha jambo linalofanya idara
kufanya kazi katika mazingira magumu.

Katika
hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Lilian Matinga na
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Enelia Lutungulu
wamewaokoa Maafisa Ardhi wa halmashauri hiyo wasitumbuliwe kutokana na
kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutokamilisha utoaji
wa hati za ardhi kwa muda mrefu.

Walionusurika
ni Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Spear
Mwalukasa ambaye ilielezwa yuko katika mafunzo  na  Afisa Ardhi Ezekiel
Bichuro. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula alisema kutokana na Maafisa hao kuzembea kukamilisha
hati kwa muda mrefu basi hawafai kuendelea na nafasi zao kwa kuwa
wanakwamisha utoaji hati ambao sasa unaweza kufanyika ndani ya mwezi
mmoja pale taratibu zote zinapokuwa zimekamilika.

Hata
hivyo, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi
Enelia Lutungulu waliwatetea kwa kueleza kuwa maafisa hao hawana muda
mrefu katika idara hiyo na makosa yanaweza kuwa yalifanywa maafisa
waliopita.

Naibu
Waziri Mabula alielekeza maafisa hao kupewa barua za onyo kwa kuwa muda
wa miezi mitatu waliopo katika idara hiyo wangeweza kuonesha jitihada
za kukamilisha hati na kuagiza hati zilizopo zikamilishwe katika kipindi
cha mwezi mmoja.

‘’Ikifika
tarehe 30 Januari 2020 hati ziwe zimeenda kwa wenyewe, haiwezekani mtu
amesaini tangu 2015 halafu mpaka sasa hajapatiwa hati yake, wapo wazembe
wachache  wanaochafua Wizara lazima wapewe warning. Alisema Naibu
Waziri Mabula.

Naibu
Waziri Mabula pia alitembelea wilaya ya Tanganyika ambapo alionesha
kutoridhika na kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la
ardhi na kuagiza halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kuongeza kasi
katika makusanyo sambamba na kupanga, kupima na kumilikisha viwanja kwa
wananchi.

Kwa
mujibu wa Afisa Ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Penina
Simon kiasi cha shilingi milioni 18,069,179.40 kilikusanywa hadi kufikia
nusu ya mwaka wa fedha 2019/2020.