Idadi ya maambukizi ya corona nchini kenya yafika 42

Watu
wanne zaidi wameambukizwa virusi vya Corona nchini Kenya na kufikisha
idadi ya wagonjwa kufikia 42, wakati huu serikali nchini humo ikiendelea
kutekeleza amri ya watu kutotoka nje, ambayo imeathiri shughuli za
biashara.


Waziri
wa afya Mutahi Kagwe amesema kuwa watatu walioambukizwa ni raia wa
Marekani, Cameroon na Burkina Faso, huku mmoja akiwa raia wa Kenya.

Maambukizi
matatu yameripotiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi na moja jijini
Mombasa. watu 1,426 waliotangamana na ambao wanashukiwa kuambukizwa
virusi hivyo wanatafutwa.

Hata
hivyo wataalamu wa afya wanasema licha ya mikakati muhimu iliyotangazwa
na Serikali kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, vita ya kuukabili itakuwa
ngumu ikiwa wananchi hawataendelea kuelimishwa kuzingatia usafi na njia
za kujikinga.

Kenya
kwa sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwatafuta watu
waliotangamana na watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Hivi
karibuni msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, alitoa wito kwa watu ambao
huenda walitangamana na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo kufika
katika kituo cha afya kilicho karibu nao.