Serikali yatoa onyo kali kwa watendaji kata


WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari
nchini ambao wamekuwa wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu
waliowapa ujauzito wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa
hatua kali za kisheria.

Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akihutubia
wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilula
Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani Kilolo akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoani Iringa.

“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa ujauzito na kukatishwa masomo yao
huku watu waliohusika na vitendo hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua
stahiki kwa sababu baadhi ya watendaji na askari wamezikalia kesi zao na
kushindwa kuwafikisha polisi.”

“Watoto wa kike lazima walindwe ili wamalize masomo yao waje kulitumikia
Taifa lao. Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo
ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na
aondokane na utegemezi.”

Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii
na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu
atakayemuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika
nyumba ya wageni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi hususan waishio
vijijini wasikubali kurubuniwa na kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali
wanaofika kwenye maeneo yao na kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha
mamlaka husika.

“Eneo lenu hili la Ilula ni zuri hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi
yenu kwa sababau inathamani kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji
hakikisheni mnaratibu vizuri na muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi
ili kuepuka migogoro.”

Waziri Mkuu alisema wananchi hao wanatakiwa wawe makini na ardhi na
mamlaka zinazohusika na ardhi lazima zihusishwe katika ugawaji wa ardhi
kwa sababu wakigawa hovyo watasababisha vijana wao hapo baadaye wakose
maeneo ya kilimo.

Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu ameahidi
ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Ilula ili kuwapunguzia wananchi
kutembea umbali mrefu hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma
hizo.

Alisema kituo kitakachojengwa kitakuwa na chumba cha kujifungulia,
chumba cha maabara kwa ajili ya vipimo mbalimbali, huduma za mama na
mtoto, mapasuaji, wodi ya wanaume na wanawake, aliwataka wananchi
waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri Mkuu alisema suala la kuboresha na kusogeza huduma mbalimbali za
kijamii kwa wananchi zikiwemo za afya limepewa kipaumbele na Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye anataka
kuona wananchi wakiwa na afya nzuri ili waweze kushiriki ipasavyo katika
shughuli zao za kimaendeleo.

Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu
alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula na kuweka jiwe la msingi. Pia,
Waziri Mkuu alikagua shughuli za ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya
Wananchi  Ilula.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege
aliwahimiza wananchi hao wajiunge katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)
ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu ya bure wao na familia
zao.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi alisema kuwa awali eneo la Ilula
lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo yam ogogoro ya
ardhi ambayo kwa kushirikiana na watendaji wenzake walifanikiwa
kuitatua.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,